7 Basi kulikuwa hapo siku hiyo mtumishi mmoja wa Shauli ambaye alikuwa amezuiliwa mbele ya Mwenyezi-Mungu. Mtumishi huyo aliitwa Doegi, Mwedomu, msimamizi wa wachungaji wa Shauli.
8 Basi, Daudi akamwambia Ahimeleki, “Je, una upanga au mkuki ambao unaweza kunipatia? Kwa kuwa shughuli za mfalme zilinilazimu niondoke haraka, nami niliondoka bila upanga wangu wala silaha nyingine yoyote.”
9 Ahimeleki akamjibu, “Ninao ule upanga wa Mfilisti Goliathi uliyemuua kwenye bonde la Ela; uko nyuma ya kizibao cha kuhani umefungwa katika kitambaa. Ikiwa unataka kuuchukua huo basi, uchukue kwani hakuna upanga mwingine hapa.” Daudi akamwambia, “Hakuna upanga mwingine kama huo; nakuomba unipe.”
10 Siku hiyo, Daudi alimkimbia Shauli, akaenda kwa mfalme Akishi wa Gathi.
11 Watumishi wa mfalme wakamwambia Akishi, “Huyu si Daudi, mfalme wa nchi ya Israeli? Je, si huyu ambaye walikuwa wakiimbiana juu yake katika ngoma, wakisema, ‘Shauli ameua maelfu yake na Daudi ameua makumi elfu yake?’”
12 Maneno hayo Daudi hakuweza kuyasahau, akaanza kumwogopa sana Akishi mfalme wa Gathi.
13 Hivyo, akabadilisha tabia yake, akijifanya mwendawazimu, akawa anakwaruzakwaruza kwenye malango ya mji, na mate yake akayaacha yatiririke kwenye ndevu zake.