5 Basi, Daudi akaenda Keila pamoja na watu wake, na huko akapigana na Wafilisti, akawaua Wafilisti wengi na kuteka nyara ng'ombe wengi. Hivyo Daudi aliwaokoa wakazi wa Keila.
6 Abiathari, mwana wa Ahimeleki, alipokimbilia kwa Daudi huko Keila, alikwenda na kizibao cha kuhani.
7 Shauli alipoambiwa kuwa Daudi amekwisha fika Keila, akasema, “Mungu amemtia mikononi mwangu kwani amejifungia mwenyewe kwa kuingia katika mji wenye malango yenye makomeo.”
8 Hivyo, Shauli aliyaita majeshi yaende Keila na kufanya mashambulizi, ili kumzingira Daudi pamoja na watu wake.
9 Daudi aliposikia mipango miovu ya Shauli dhidi yake, akamwambia kuhani Abiathari, “Kilete hapa hicho kizibao cha kuhani.”
10 Kisha Daudi akaomba, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa hakika mimi mtumishi wako, nimesikia kwamba Shauli anapanga kuja kuangamiza mji wa Keila kwa sababu yangu.
11 Je, wakazi wa Keila watanitia mikononi mwa Shauli? Je, Shauli atakuja kweli kama nilivyosikia mimi mtumishi wako? Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nakuomba unijibu mimi mtumishi wako.”Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Shauli atakuja.”