1 Baada ya muda fulani, Wafilisti walikusanya majeshi yao tayari kwenda kupigana na Waisraeli. Akishi akamwambia Daudi, “Uelewe vizuri kwamba wewe na watu wako mnapaswa kwenda pamoja nami kupigana vita.”
2 Daudi akamjibu Akishi, “Naam! Utaona kitu ambacho mtumishi wako anaweza kufanya.” Akishi akamwambia, “Nami nitakufanya kuwa mlinzi wangu binafsi wa maisha.”
3 Wakati huu, Samueli alikuwa amekwisha fariki, na Waisraeli wote walikuwa wamekwisha mwombolezea na kumzika katika mji wake Rama. Shauli alikuwa amewafukuza kutoka nchini watabiri na wachawi.
4 Wafilisti walikusanyika na kupiga kambi yao huko Shunemu; na Shauli aliwakusanya Waisraeli wote na kupiga kambi yao kwenye mlima Gilboa.