10 Walifanya kama walivyoambiwa; waliwachukua ng'ombe wawili wanaokamuliwa na kuwafunga kwenye gari, na ndama wao wakawafunga zizini.
11 Lile sanduku la Mwenyezi-Mungu wakalitia kwenye gari hilo pamoja na lile kasha lenye vinyago vya dhahabu vya panya na vile vya majipu.
12 Hao ng'ombe walikwenda moja kwa moja kuelekea mji wa Beth-shemeshi bila kupinda kushoto au kulia, na walikuwa wanalia walipokuwa wanakwenda. Wale wafalme watano wa Wafilisti waliwafuata hadi mpakani mwa Beth-shemeshi.
13 Watu wa Beth-shemeshi walikuwa wanavuna ngano bondeni. Walipotazama juu na kuliona sanduku la Mwenyezi-Mungu, wakafurahi sana.
14 Hilo gari lilielekea kwenye shamba la Yoshua, mkazi wa Beth-shemeshi. Lilipofika hapo likasimama karibu na jiwe kubwa. Watu wakalibomoa lile gari, wakatumia mbao zake kwa kuwateketeza hao ng'ombe ambao waliwatoa kama sadaka ya kuteketezwa kwa Mwenyezi-Mungu.
15 Walawi walikuwa wameliteremsha sanduku la Mwenyezi-Mungu na lile kasha lenye vinyago vya dhahabu na kuviweka kwenye lile jiwe kubwa. Basi, siku hiyo watu wa Beth-shemeshi walitoa sadaka za kuteketezwa, na kumtolea tambiko Mwenyezi-Mungu.
16 Wale wakuu watano wa Wafilisti walipoona hayo, walirudi Ekroni, siku hiyohiyo.