1 Samueli 6:14-20 BHN

14 Hilo gari lilielekea kwenye shamba la Yoshua, mkazi wa Beth-shemeshi. Lilipofika hapo likasimama karibu na jiwe kubwa. Watu wakalibomoa lile gari, wakatumia mbao zake kwa kuwateketeza hao ng'ombe ambao waliwatoa kama sadaka ya kuteketezwa kwa Mwenyezi-Mungu.

15 Walawi walikuwa wameliteremsha sanduku la Mwenyezi-Mungu na lile kasha lenye vinyago vya dhahabu na kuviweka kwenye lile jiwe kubwa. Basi, siku hiyo watu wa Beth-shemeshi walitoa sadaka za kuteketezwa, na kumtolea tambiko Mwenyezi-Mungu.

16 Wale wakuu watano wa Wafilisti walipoona hayo, walirudi Ekroni, siku hiyohiyo.

17 Wafilisti walivipeleka vile vinyago vitano vya dhahabu na vya majipu kwa Mwenyezi-Mungu vikiwa sadaka ya kuondoa hatia yao, kinyago kimoja kwa ajili ya mji mmoja: Mji wa Ashdodi, mji wa Gaza, mji wa Ashkeloni, mji wa Gathi na kwa mji wa Ekroni.

18 Walipeleka pia vinyago vitano vya dhahabu vya panya kulingana na hesabu ya miji yote ya Wafilisti iliyotawaliwa na wakuu watano wa Wafilisti. Miji hiyo ilikuwa yenye ngome na vijiji ambavyo havikuzungushiwa kuta. Lile jiwe kubwa kwenye shamba la Yoshua wa Beth-shemeshi, mahali ambapo walilipeleka sanduku la Mwenyezi-Mungu, ni ushahidi wa tukio hilo hadi leo.

19 Mwenyezi-Mungu aliwaua wakazi sabini wa mji wa Beth-shemeshi, kwa sababu waliangalia ndani ya sanduku lake. Watu waliomboleza kwa sababu Mwenyezi-Mungu alikuwa amefanya mauaji makubwa miongoni mwao.

20 Kisha, wakazi wa mji wa Beth-shemeshi wakasema: “Nani awezaye kusimama mbele ya Mwenyezi-Mungu, huyu Mungu mtakatifu? Atakwenda kwa nani ili aondoke kwetu?”