2 Wafilisti waliwaita makuhani na waaguzi wao na kuwauliza, “Tufanyeje na sanduku hili la Mwenyezi-Mungu? Tuambieni namna gani tunavyoweza kulirudisha mahali pake.”
3 Wao wakawaambia, “Mkirudisha sanduku la Mungu wa Israeli, msilirudishe mikono mitupu. Lakini kwa vyovyote vile mnapolirudisha pelekeni na sadaka ya kuondoa hatia ili kuondoa hatia yenu. Mkifanya hivyo mtapona, nanyi mtafahamu kwa nini amekuwa akiwaadhibu mfululizo.”
4 Watu wakauliza, “Tutampelekea sadaka gani ya kuondoa hatia?” Wao wakawajibu “Vinyago vitano vya dhahabu vilivyo mfano wa majipu, na vinyago vitano vya dhahabu vikiwa mfano wa panya, kila kimoja kikiwakilisha mkuu mmoja wa Wafilisti, kwani tauni iliyotumwa kwenu ni ileile iliyotumwa kwa wakuu wenu.
5 Lazima mfanye vinyago vya majipu na vinyago vya panya wenu, vitu ambavyo vinaangamiza nchi yenu. Ni lazima mumpe heshima Mungu wa Israeli. Labda ataacha kuwaadhibu, nyinyi wenyewe, miungu yenu na nchi yenu.
6 Kwa nini mnakuwa wakaidi kama Wamisri na Farao? Je, Mungu alipowadhihaki Wamisri, hawakuwaacha Waisraeli waondoke, nao wakaondoka?
7 Basi, tayarisheni gari jipya na ng'ombe wawili wakamuliwao ambao bado hawajafungwa nira; wafungeni kwenye gari hilo lakini ndama wao wasiende pamoja nao, ila wabaki zizini.
8 Chukueni sanduku la Mwenyezi-Mungu na kuliweka katika gari hilo. Kando ya sanduku wekeni vile vinyago vya dhahabu ambavyo mnampelekea kama sadaka ya kuondoa hatia yenu. Kisha mliache liende litakakokwenda.