1 Baadaye, mnamo mwaka wa saba, kuhani Yehoyada alijipa moyo akafanya mapatano na makapteni: Azaria mwana wa Yehoramu, Ishmaeli mwana wa Yehohanani, Azaria mwana wa Obedi, Maaseya mwana wa Adaya, na Elishafati mwana wa Zikri.
2 Wakazunguka katika miji yote ya Yuda wakiwakusanya Walawi na viongozi wa makabila ya Israeli, wakaenda mpaka Yerusalemu.
3 Mkutano wote ukafanya agano na mfalme katika nyumba ya Mungu. Yehoyada akawaambia, “Mwangalie huyu mwana wa mfalme! Mwacheni atawale kulingana na ahadi aliyoitoa Mwenyezi-Mungu kuhusu uzao wa Daudi.
4 Hivi ndivyo mtakavyofanya: Theluthi moja yenu nyinyi makuhani na Walawi mtakaoshika zamu siku ya Sabato, mtayalinda malango,
5 theluthi nyingine italinda ikulu na theluthi iliyobakia mtalinda Lango la Msingi. Watu wote watakuwa katika nyua za nyumba ya Mwenyezi-Mungu.
6 Asikubaliwe mtu mwingine yeyote kuingia nyumba ya Mwenyezi-Mungu isipokuwa makuhani tu pekee na wale Walawi watakaokuwa wanahudumu. Hao wanaweza kuingia kwa sababu wao ni watakatifu, lakini wale watu wengine wote, watatii amri ya Mwenyezi-Mungu.
7 Walawi watamzunguka mfalme, kila mtu na silaha yake mkononi; na mtu yeyote atakayejaribu kuingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, atauawa. Mkae na mfalme popote aendapo.”