15 Siku ya kumi na nne ya mwezi huo walichinja mwanakondoo wa Pasaka. Makuhani na Walawi waliona aibu, wakajitakasa na kuleta sadaka za kuteketeza katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.
16 Walichukua nafasi zao hekaluni kulingana na maagizo yaliyokuwamo katika sheria za Mose, mtu wa Mungu. Walawi waliwapa makuhani damu ya tambiko, nao wakainyunyiza madhabahuni.
17 Kwa vile wengi wa wale waliokusanyika hapo hawakuwa wamejitakasa, iliwabidi Walawi kuwachinjia wanakondoo wa Pasaka na kuwaweka wakfu kwa Mwenyezi-Mungu.
18 Aidha miongoni mwa kusanyiko hilo la watu, wengi wa wale waliotoka Efraimu, Manase, Isakari na Zebuluni, walikuwa wakiiadhimisha Pasaka kinyume cha maagizo. Hii ni kwa kuwa mfalme Hezekia aliwaombea akisema, “Mwenyezi-Mungu uliye mwema, msamehe yeyote yule
19 atakayekuomba kwa moyo wake wote wewe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zake, hata ingawa si msafi kulingana na sheria za utakaso.”
20 Mwenyezi-Mungu alikubali ombi la Hezekia, akawasamehe watu hao.
21 Waisraeli wote waliokuwa wamekusanyika mjini Yerusalemu waliiadhimisha sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu kwa muda wa siku saba, wakiwa na furaha kubwa. Walawi na makuhani walimsifu Mwenyezi-Mungu kila siku, walimwimbia kwa nguvu zao zote.