1 Baada ya sherehe kumalizika, watu wote wa Israeli walikwenda katika kila mji wa Yuda, wakavunjavunja nguzo za mawe na kuzikatakata sanamu za Ashera, mungu wa kike, na pia wakaziharibu madhabahu na mahali pa kuabudia miungu mingine. Walifanya vivyo hivyo kote katika Yuda, Benyamini, Efraimu na Manase, mpaka walipokwisha kuharibu vyote. Kisha wakarudi mjini mwao, kila mtu kwenye milki yake.
2 Mfalme Hezekia aliwapanga tena makuhani na Walawi katika makundi, akampa kila mmoja wao wajibu maalumu, kuhudumu katika sehemu mbalimbali za hekalu la Mwenyezi-Mungu. Wajibu huo ni pamoja na utoaji wa sadaka za kuteketeza na za amani, kushukuru na kusifu.
3 Kutokana na mali yake mwenyewe, mfalme alitoa sehemu kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa asubuhi na jioni, sadaka za siku ya Sabato na wakati wa sherehe za kuadhimisha mwezi mwandamo na zile sikukuu nyingine zilizoamriwa kulingana na sheria ya Mwenyezi-Mungu.
4 Zaidi ya hayo, mfalme aliwaambia wenyeji wa Yerusalemu watoe sehemu waliyostahili kupewa makuhani na Walawi, ili wao wajitolee kikamilifu katika shughuli za sheria za Mwenyezi-Mungu.
5 Mara tu amri hii ilipotolewa, watu wa Israeli walitoa kwa wingi, malimbuko ya nafaka, divai, mafuta, asali na mazao mengine mbalimbali ya shambani, na pia zaka nyingi za kila kitu.
6 Watu wa Israeli na Yuda walioishi katika miji ya Yuda, pia wakaleta zaka zao za ng'ombe na kondoo na vitu vingine, wakaviweka wakfu kwa Mwenyezi-Mungu. Waliviweka vitu hivyo katika mafungu.