8 Na iwapo watu wa Israeli watajali kutenda yote niliyowaamuru, wakatii sheria zote, masharti, na maagizo yaliyotolewa kwa mkono wa Mose, basi kamwe sitawaacha wafukuzwe kutoka katika nchi hii ambayo niliwapa babu zao.”
9 Lakini Manase aliwapotosha watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu, wakatenda maovu zaidi kuliko mataifa ambayo Mwenyezi-Mungu aliyaangamiza mbele ya watu wa Israeli.
10 Mwenyezi-Mungu alimwonya Manase na watu wake, lakini hawakumsikia.
11 Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu akawaleta makamanda wa jeshi la mfalme wa Ashuru. Hao makamanda walimkamata Manase kwa kulabu wakamfunga pingu za shaba, wakampeleka hadi Babuloni.
12 Wakati alipokuwa taabuni, alimwomba Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, akajinyenyekesha sana mbele ya Mungu wa babu zake.
13 Alimsihi, naye Mungu akapokea ombi lake na sala yake akamrudisha Yerusalemu katika ufalme wake. Ndipo Manase akatambua kuwa Mwenyezi-Mungu ndiye Mungu.
14 Baada ya haya, Manase alijenga ukuta mwingine upande wa nje wa mji wa Daudi, magharibi mwa Gihoni, bondeni, akauendeleza hadi Lango la Samaki, akauzungusha hadi Ofeli; akauinua juu sana. Pamoja na hayo, aliweka makamanda wa majeshi katika miji yote ya Yuda yenye ngome.