17 Wakamchukua Absalomu wakamtupa kwenye shimo kubwa msituni na kurundika rundo kubwa sana la mawe. Watu wote wa Israeli wakakimbia, kila mmoja nyumbani kwake.
18 Absalomu, wakati wa uhai wake, alikuwa amejijengea na kujisimikia nguzo iliyoko kwenye Bonde la Mfalme, kwani alisema, “Mimi sina mtoto wa kiume wa kudumisha jina langu ili nikumbukwe.” Nguzo hiyo aliipa jina lake, na inaitwa “Nguzo ya Absalomu” mpaka leo.
19 Kisha, Ahimaasi mwana wa Sadoki, akasema, “Niruhusu nikimbie kumpelekea mfalme habari hizi kuwa Mwenyezi-Mungu amemkomboa katika nguvu za adui zake.”
20 Yoabu akamwambia, “Leo, hutapeleka habari hizo. Unaweza kupeleka habari hizo siku nyingine. Lakini leo hutapeleka habari zozote kwa kuwa mwana wa mfalme amekufa.”
21 Ndipo Yoabu akamwambia mtu mmoja, Mkushi, “Wewe, nenda ukamweleze mfalme yale uliyoona.” Mkushi akainama kwa heshima mbele ya Yoabu, akaondoka mbio.
22 Kisha Ahimaasi mwana wa Sadoki akamwambia Yoabu tena, “Haidhuru; niruhusu na mimi nimkimbilie yule Mkushi!” Yoabu akamwambia, “Mbona unataka kukimbia mwanangu? Wewe hutatuzwa lolote kwa habari hizi!”
23 Ahimaasi akamwambia, “Haidhuru; nitakimbia.” Basi, Yoabu akamwambia, “Haya, kimbia.” Kisha Ahimaasi akakimbia akifuata njia ya nyikani akawahi kumpita yule Mkushi.