11 Mtu mmoja wa Yoabu akaja akasimama karibu na mwili wa Amasa, akasema, “Yeyote anayempenda Yoabu na yeyote anayempenda Daudi, na amfuate Yoabu!”
12 Amasa alikuwa bado anagagaa kwenye damu yake katikati ya barabara kuu. Kwa hiyo, kila mtu aliyepita hapo, alipomwona, alisimama. Lakini yule mtu alipoona kwamba watu wote walikuja na kusimama hapo, aliuondoa mwili wa Amasa barabarani, akaupeleka shambani na kuufunika kwa nguo.
13 Amasa alipoondolewa kwenye barabara kuu, watu wote sasa waliendelea kumfuata Yoabu kumfuatia Sheba mwana wa Bikri.
14 Sheba alipitia katika makabila yote ya Israeli mpaka mji wa Abeli wa Beth-maaka. Watu wote wa ukoo wa Bikri wakakusanyika na kumfuata.
15 Watu wote waliokuwa pamoja na Yoabu wakaenda kumzingira Sheba akiwa katika mji huo wa Abeli wa Beth-maaka. Walirundika kuuzingira mji, na ngome; halafu wakaanza kuubomoa ukuta ili kuuangusha chini.
16 Kisha, mwanamke fulani mwenye hekima alisikika kutoka mjini akisema, “Sikieni! Sikieni! Mwambieni Yoabu aje nizungumze naye.”
17 Yoabu akaenda karibu naye, huyo mwanamke akamwambia, “Je, wewe ni Yoabu?” Yoabu akasema, “Naam! Ni mimi.” Yule mwanamke akamwambia, “Nisikilize mimi mtumishi wako.” Yoabu akamwambia, “Nasikiliza.”