3 Hata hivyo, mahali pa juu pa kuabudia miungu hapakuharibiwa, na watu waliendelea kutambika na kufukiza ubani huko.
4 Yoashi akaita makuhani na kuwaamuru, akisema, “Fedha yote inayoletwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu ikiwa imetokana na uuzaji wa vitu vitakatifu, fedha ya kila mtu kadiri alivyoandikiwa, na fedha ambayo mtu huvutwa kuitoa kwa hiari katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu,
5 makuhani wazipokee kutoka kwa kila mtu; nao warekebishe nyumba popote panapohitajika marekebisho.”
6 Lakini hata baada ya miaka ishirini na mitatu ya mfalme Yoashi makuhani walikuwa bado hawajafanya marekebisho yoyote ya nyumba.
7 Kwa hiyo mfalme Yoashi alimwita kuhani Yehoyada na makuhani wengine na kuwauliza, “Mbona hamrekebishi nyumba? Basi, msichukue fedha kutoka kwa watu mnaowatumikia, bali mtazileta, ili nyumba irekebishwe.”
8 Makuhani wakakubali wasipokee fedha tena kutoka kwa watu na pia wakaahidi kutofanya marekebisho ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu.
9 Yehoyada akachukua sanduku na kutoboa tundu kwenye kifuniko chake, kisha akaliweka kwenye madhabahu upande wa kulia, mtu anapoingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Nao makuhani waliokuwa katika zamu langoni waliweka fedha zote zilizoletwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.