1 Katika mwaka wa kumi na mbili wa enzi ya mfalme Ahazi wa Yuda, Hoshea mwana wa Ela alianza kutawala Israeli, akatawala huko Samaria kwa miaka tisa.
2 Alitenda dhambi mbele ya Mwenyezi-Mungu ingawa siyo kama wafalme wa Israeli waliomtangulia.
3 Mfalme Shalmanesa wa Ashuru alimshambulia; naye Hoshea akawa mtumishi wake na kumlipa ushuru.
4 Lakini wakati mmoja Hoshea alituma wajumbe kwa mfalme wa Misri akiomba msaada; ndipo akaacha kulipa ushuru kwa mfalme Shalmanesa wa Ashuru kama alivyozoea kufanya kila mwaka. Shalmanesa alipoona hivi alimfunga Hoshea kwa minyororo na kumweka gerezani.
5 Kisha mfalme wa Ashuru akaivamia nchi nzima na kuufikia mji wa Samaria na kuuzingira kwa muda wa miaka mitatu.