1 Katika mwaka wa kumi na mbili wa enzi ya mfalme Ahazi wa Yuda, Hoshea mwana wa Ela alianza kutawala Israeli, akatawala huko Samaria kwa miaka tisa.
2 Alitenda dhambi mbele ya Mwenyezi-Mungu ingawa siyo kama wafalme wa Israeli waliomtangulia.
3 Mfalme Shalmanesa wa Ashuru alimshambulia; naye Hoshea akawa mtumishi wake na kumlipa ushuru.
4 Lakini wakati mmoja Hoshea alituma wajumbe kwa mfalme wa Misri akiomba msaada; ndipo akaacha kulipa ushuru kwa mfalme Shalmanesa wa Ashuru kama alivyozoea kufanya kila mwaka. Shalmanesa alipoona hivi alimfunga Hoshea kwa minyororo na kumweka gerezani.
5 Kisha mfalme wa Ashuru akaivamia nchi nzima na kuufikia mji wa Samaria na kuuzingira kwa muda wa miaka mitatu.
6 Katika mwaka wa tisa wa utawala wa Hoshea, mfalme wa Ashuru aliuteka Samaria, na kuwachukua watu wa Israeli mateka mpaka Ashuru, baadhi yao akawaweka katika mji wa Hala, wengine karibu na mto Habori, mto Gozani na wengine katika miji ya Media.
7 Haya yote yalitendeka kwa sababu watu wa Israeli walimwasi Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, ambaye aliwatoa kutoka mikononi mwa mfalme wa Misri, pia waliabudu miungu mingine,