23 hadi hatimaye Mwenyezi-Mungu akawafukuza kutoka mbele yake, kama vile alivyokuwa amesema kupitia kwa watumishi wake wote manabii. Kwa hiyo watu wa Israeli walichukuliwa mateka kutoka nchi yao wenyewe mpaka Ashuru ambako wanakaa hata sasa.
24 Kisha mfalme wa Ashuru akachukua watu kutoka Babuloni, Kutha, Ava, Hamathi na Sefarvaimu na kuwaweka katika miji ya Samaria mahali pa watu wa Israeli waliopelekwa uhamishoni. Wakaitwaa miji hiyo na kukaa humo.
25 Basi ilitokea kwamba walipoanza kukaa humo, hawakumwabudu Mwenyezi-Mungu, kwa hiyo Mwenyezi-Mungu akatuma simba miongoni mwao, nao wakawaua baadhi yao.
26 Halafu watu walimwambia mfalme wa Ashuru, “Mataifa uliyochukua na kuyaweka katika miji ya Samaria hayakujua hukumu za Mungu wa nchi hiyo, kwa hiyo Mungu huyo alituma simba ambao wanawaua.”
27 Ndipo mfalme wa Ashuru akaamuru, “Mrudishe kuhani mmoja kati ya wale tuliowaleta mateka; mrudishe aende na kukaa huko, ili awafundishe watu sheria ya Mungu wa nchi hiyo.”
28 Kwa hiyo mmoja wa makuhani waliotekwa nyara toka Samaria alikwenda na kukaa Betheli, na huko aliwafundisha watu jinsi ya kumwabudu Mwenyezi-Mungu.
29 Lakini mataifa yote katika miji yalimoishi yalijitengenezea miungu yao na kuiweka mahali pa juu ambako watu wa Samaria walikuwa wametengeneza.