18 Kisha wakarudi kwa Elisha aliyekuwa anawangojea huko Yeriko. Elisha akawauliza, “Je, sikuwaambieni msiende?”
19 Baadaye watu wa Yeriko walimwendea Elisha, wakamwambia, “Bwana, kama uonavyo mji huu ni mzuri, lakini maji tuliyo nayo ni mabaya na yanasababisha mimba kuharibika.”
20 Elisha akawaambia, “Tieni chumvi ndani ya bakuli jipya, kisha mniletee.” Nao wakamletea.
21 Elisha akaenda kwenye chemchemi ya maji, akatupa chumvi hiyo ndani na kusema, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: Nimeyafanya maji haya kuwa yenye kufaa; tangu sasa hayatasababisha vifo au kutoa mimba.”
22 Na maji hayo yamekuwa ya kufaa mpaka leo, kama alivyosema Elisha.
23 Elisha aliondoka Yeriko, akaenda Betheli. Alipokuwa njiani, vijana fulani walitoka mjini wakaanza kumzomea wakisema, “Nenda zako, nenda zako mzee kipara!”
24 Elisha aligeuka akawatazama na kuwalaani kwa jina la Mwenyezi-Mungu. Dubu wawili majike wakatoka mwituni, wakawararua vijana arubaini na wawili miongoni mwao.