7 Watu wanaosimamia ujenzi wasidaiwe kutoa hesabu ya matumizi ya fedha watakazokabidhiwa, kwa sababu wanazitumia kwa uaminifu.”
8 Kisha kuhani mkuu Hilkia alimwambia katibu Shafani, “Nimekipata Kitabu cha Sheria katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.” Halafu Hilkia akampatia Shafani kitabu, naye akakisoma.
9 Katibu Shafani, alimwendea mfalme na kutoa habari, akisema, “Watumishi wako wametoa fedha zilizopatikana katika nyumba halafu wamezikabidhi kwa mafundi wanaosimamia marekebisho ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu.”
10 Kisha katibu Shafani, akamwambia mfalme, “Kuhani Hilkia amenipa kitabu.” Naye Shafani akakisoma mbele ya mfalme.
11 Mfalme aliposikia maneno ya Kitabu cha Sheria, alirarua mavazi yake.
12 Mara aliamuru kuhani Hilkia, Ahikamu mwana wa Shafani na Akbori mwana wa Mikaya pamoja na katibu Shafani na Asaya mtumishi wa mfalme, akisema,
13 “Nendeni mkatafute shauri kutoka kwa Mwenyezi-Mungu kwa niaba yangu na watu wa Yuda wote kuhusu maneno ya kitabu hiki kilichopatikana kwa sababu ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu imewaka juu yetu, maana babu zetu hawakutii maneno ya kitabu hiki, na kutimiza yote yaliyoandikwa kutuhusu.”