9 Katibu Shafani, alimwendea mfalme na kutoa habari, akisema, “Watumishi wako wametoa fedha zilizopatikana katika nyumba halafu wamezikabidhi kwa mafundi wanaosimamia marekebisho ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu.”
10 Kisha katibu Shafani, akamwambia mfalme, “Kuhani Hilkia amenipa kitabu.” Naye Shafani akakisoma mbele ya mfalme.
11 Mfalme aliposikia maneno ya Kitabu cha Sheria, alirarua mavazi yake.
12 Mara aliamuru kuhani Hilkia, Ahikamu mwana wa Shafani na Akbori mwana wa Mikaya pamoja na katibu Shafani na Asaya mtumishi wa mfalme, akisema,
13 “Nendeni mkatafute shauri kutoka kwa Mwenyezi-Mungu kwa niaba yangu na watu wa Yuda wote kuhusu maneno ya kitabu hiki kilichopatikana kwa sababu ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu imewaka juu yetu, maana babu zetu hawakutii maneno ya kitabu hiki, na kutimiza yote yaliyoandikwa kutuhusu.”
14 Kwa hiyo kuhani Hilkia, Ahikamu, Akbori, Shafani na Asaya, wote walikwenda kwa mama mmoja nabii jina lake Hulda aliyekuwa mke wa Shalumu, mwana wa Tikva, mwana wa Harhasi, mtunza mavazi ya hekalu. Wakati huo Hulda alikuwa anaishi katika mtaa wa pili wa Yerusalemu, nao wakazungumza naye.
15 Basi akawaambia, “Hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli: ‘Mwambie huyo aliyewatuma kwangu,