11 Kadhalika aliondoa farasi waliotengwa na wafalme wa Yuda kwa ajili ya jua, kwenye njia ya kuingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, karibu na chumba cha Nathan-meleki, kilichokuwa kiungani; naye alichoma kwa moto magari ya jua.
12 Madhabahu ambayo wafalme wa Yuda walijenga paani kwenye chumba cha juu cha Ahazi, pamoja na madhabahu ambayo Manase alijenga katika nyua mbili za nyumba ya Mwenyezi-Mungu aliyabomoa na kuyapondaponda, kisha alitupa mavumbi yake katika kijito cha Kidroni.
13 Mfalme pia alipatia unajisi mahali pa kuabudia palipokuwa upande wa mashariki ya Yerusalemu na kuelekea upande wa mlima wa Ufisadi, mahali mfalme wa Israeli alipopajenga kwa ajili ya Ashtarothi chukizo la Wasidoni, Kemoshi chukizo la Moabu na pia kwa ajili ya Milkomu chukizo la Waamoni.
14 Alivunja nguzo katika vipandevipande; pia alikatakata sanamu za Ashera, na mahali zilipokuwa zinasimama alipajaza mifupa ya watu.
15 Zaidi ya hayo aliharibu huko Betheli mahali pa kuabudia palipojengwa na mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati, aliyewafanya watu wa Israeli watende dhambi; aliharibu madhabahu hayo na kuvunja mawe yake katika vipandevipande, na kisha akaviponda mpaka vikawa vumbi; pia akachoma sanamu ya Ashera.
16 Kisha Yosia alipogeuka aliona makaburi juu ya kilima; aliagiza mifupa ifukuliwe kutoka makaburini na kuichoma juu ya madhabahu; basi akayatia unajisi madhabahu sawasawa na neno la Mwenyezi-Mungu ambalo mtu wa Mungu alilitangaza, nabii ambaye alitabiri matukio haya.
17 Halafu mfalme aliuliza, “Mnara ninaouona kule ni wa nini?” Nao watu wa mji wakamjibu, “Ni kaburi la mtu wa Mungu ambaye alikuja kutoka Yuda na kutabiri mambo ambayo umeyafanya dhidi ya madhabahu pale Betheli.”