10 Wakati huo jeshi la Nebukadneza mfalme wa Babuloni, lilishambulia mji wa Yerusalemu na kuuzingira.
11 Wakati majeshi yalipokuwa yanauzingira mji, Nebukadneza mwenyewe alikuja Yerusalemu,
12 na Yehoyakini mfalme wa Yuda alijisalimisha kwa mfalme wa Babuloni, yeye mwenyewe pamoja na mama yake, watumishi wake, maofisa na maakida wake. Mfalme wa Babuloni alimchukua mateka katika mwaka wa nane wa kutawala kwake.
13 Vilevile, pia kama Mwenyezi-Mungu alivyosema, Nebukadneza alichukua mali yote iliyokuwa ndani ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, na ndani ya ikulu. Alikatakata vyombo vyote vya dhahabu ambavyo Solomoni mfalme wa Israeli alitengeneza. Vyombo hivyo vilikuwa ndani ya hekalu la Mwenyezi-Mungu.
14 Alichukua watu wote wa Yerusalemu: Wakuu wote, watu wote waliokuwa mashujaa, mateka 10,000, na mafundi wote na wahunzi. Hakuna aliyebaki isipokuwa waliokuwa maskini kabisa nchini.
15 Alimchukua Yehoyakini mpaka Babuloni pamoja na mama yake mfalme, wake za mfalme, maofisa wake na wakuu wa nchi; wote hao aliwatoa Yerusalemu, akawapeleka Babuloni.
16 Nebukadneza alichukua watu mashujaa wa Yuda jumla yao watu 7,000 pamoja na mafundi hodari na wahunzi 1,000; wote hawa wakiwa watu wenye nguvu na wa kuweza kupigana vitani.