6 Basi, Wakaldayo walimteka mfalme, wakampeleka kwa mfalme wa Babuloni huko Ribla, naye akamhukumu.
7 Halafu waliwaua wanawe akiona kwa macho yake mwenyewe, kisha wakamngoa macho yake. Mwishowe walimfunga kwa pingu, wakampeleka Babuloni.
8 Katika siku ya saba ya mwezi wa tano wa mwaka wa kumi na tisa wa utawala wa Nebukadneza mfalme wa Babuloni, Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme, aliingia Yerusalemu.
9 Aliichoma moto nyumba ya Mwenyezi-Mungu, ikulu na nyumba zote za Yerusalemu; kila nyumba kubwa aliichoma moto.
10 Nao askari wote wa Wakaldayo waliokuwa pamoja na kapteni na walinzi wa mfalme walizibomoa kuta zilizouzunguka mji wa Yerusalemu.
11 Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme, aliwapeleka uhamishoni watu waliokuwa wamebakia mjini na wale wote waliokuwa wamejisalimisha kwa mfalme wa Babuloni pamoja na watu wengine wote.
12 Lakini aliacha baadhi ya watu waliokuwa maskini kabisa nchini. Aliwaacha watunze mizabibu na kulima mashamba.