12 Yehoshafati akasema, “Huyo ni nabii wa kweli.” Kisha wafalme hao watatu wakamwendea Elisha.
13 Elisha akamwuliza mfalme wa Israeli, “Nina uhusiano gani nawe? Nenda ukawatake shauri manabii ambao baba yako na mama yako waliwaendea.” Mfalme wa Israeli akajibu, “Sivyo! Mwenyezi-Mungu ndiye aliyetuita sisi wafalme watatu ili atutie mikononi mwa mfalme wa Moabu.”
14 Elisha akasema, “Kama aishivyo Mwenyezi-Mungu mwenye nguvu ambaye mimi ninamtumikia, naapa kwamba kama isingekuwa kwa heshima niliyo nayo kwa rafiki yako mfalme Yehoshafati wa Yuda, nisingekujali hata kidogo.
15 Lakini sasa niletee mpiga kinanda.” Wakamletea mpiga kinanda. Ikawa alipopiga kinanda, nguvu ya Mwenyezi-Mungu ikamjia Elisha,
16 akasema, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Chimbeni mashimo kila mahali kote bondeni.
17 Ingawa hamtaona upepo wala mvua, bonde litajaa maji, nanyi mtakunywa, nyinyi pamoja na ng'ombe wenu na wanyama wenu.’
18 Lakini hili si jambo gumu kwa Mwenyezi-Mungu; yeye atawapeni pia ushindi juu ya Moabu.