Amosi 7 BHN

MAONO YA HUKUMU

Maono ya kwanza: Nzige

1 Siku moja, Bwana Mwenyezi-Mungu alinijalia maono: Nilimwona Mungu anaumba nzige kundi zima, mara baada ya watu kumaliza kukata nyasi kwa ajili ya wanyama wa mfalme. Wakati huo, nyasi zilikuwa ndio zinaanza kuchipua tena.

2 Niliwaona nzige hao wakila na kumaliza kila jani katika nchi. Ndipo nikasema:“Ee Bwana Mwenyezi-Mungu, nakusihi utuhurumie!Wazawa wa Yakobo watawezaje kuishi?Wao ni wadogo mno!”

3 Basi, Bwana Mwenyezi-Mungu akabadili nia yake,akasema, “Haitakuwa hivyo!”

Maono ya pili: Moto

4 Bwana Mwenyezi-Mungu alinijalia maono mengine: Nilimwona Bwana Mwenyezi-Mungu akiuita moto wa hukumu ya kuwaadhibu watu. Moto huo uliunguza vilindi vikuu vya bahari, ukaanza kuiteketeza nchi kavu.

5 Ndipo nikasema:“Ee Bwana Mwenyezi-Mungu, nakusihi uache kuadhibu!Wazawa wa Yakobo watawezaje kuishi?Wao ni wadogo mno!”

6 Basi, Mwenyezi-Mungu akabadili nia yake,akasema: “Hili pia halitatukia.”

Maono ya tatu: Timazi

7 Mwenyezi-Mungu alinijalia tena maono mengine: Nilimwona Mwenyezi-Mungu amesimama karibu na ukuta, ameshika mkononi mwake uzi wenye timazi.

8 Naye akaniuliza: “Amosi, unaona nini?” Nikamjibu, “Naona timazi.” Kisha Mwenyezi-Mungu akasema:“Tazama! Naweka timazi kati ya watu wangu Waisraeli.Sitavumilia tena maovu yao.

9 Huko vilimani ambako wazawa wa Isaka hutambikia,kutafanywa kuwa uharibifu mtupuna maskani ya Waisraeli yatakuwa magofu.Nitaushambulia kwa vita ukoo wa mfalme Yeroboamu.”

Amosi na Amazia

10 Basi, Amazia kuhani wa mji wa Betheli, akampelekea mfalme Yeroboamu wa Israeli habari hizi: “Amosi analeta fitina juu yako katika ufalme wa Israeli. Hotuba zake ni hatari kwa nchi hii.

11 Anachosema ni hiki:‘Yeroboamu atakufa kwa upanganao Waisraeli watapelekwa uhamishoni,mbali kabisa na nchi yao.’”

12 Kisha Amazia akamwambia Amosi, “Sasa tumekuchoka, ewe nabii! Nenda zako! Rudi katika nchi ya Yuda, ukatoe unabii huko upate na ujira wako hukohuko.

13 Usitoe tena unabii hapa mjini Betheli, kwa kuwa hapa ni maskani ya ibada ya mfalme; ni hekalu la utawala huu.”

14 Amosi akamjibu Amazia, “Mimi si nabii wa kuajiriwa, wala si mmoja wa kikundi cha manabii. Mimi ni mchungaji na mtunza mikuyu.

15 Mwenyezi-Mungu alinitoa katika kazi yangu hiyo ya uchungaji, akaniamuru nije kuwaambia unabii watu wake wa Israeli.

16 Nawe basi, ewe Amazia,sikiliza neno la Mwenyezi-Mungu:Wewe waniambia nisitoe unabii dhidi ya Israeli,wala nisihubiri dhidi ya wazawa wa Isaka.

17 Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu asema hivi:‘Mkeo atakuwa malaya mjini,na wanao wa kiume na kike watauawa vitani.Ardhi yako itagawanywa na kupewa wengine,nawe binafsi utafia katika nchi najisi,nao Waisraeli hakika watapelekwa uhamishoni,mbali kabisa na nchi yao.’”

Sura

1 2 3 4 5 6 7 8 9