4 Kisha utatengeneza wavu wa shaba wenye pete nne za shaba kwenye pembe zake nne.
5 Wavu huo utauweka kwenye ukingo wa madhabahu upande wa chini ili ufike katikati ya madhabahu.
6 Utatengeneza pia mipiko ya mjohoro ya kuibebea madhabahu; nayo utaipaka shaba.
7 Mipiko hiyo itaingizwa kwenye zile pete kila upande wa madhabahu, wakati wa kuibeba.
8 Utaitengeneza madhabahu kwa mbao, na iwe yenye mvungu ndani, kulingana na mfano niliokuonesha mlimani.
9 “Utatengeneza ua wa hema la mkutano. Upande wa kusini wa ua kutakuwa na vyandarua vilivyotengenezwa kwa kitani safi iliyosokotwa ambavyo vitakuwa na urefu wa mita 44 kwa upande mmoja.
10 Vyandarua hivyo vitashikiliwa na nguzo ishirini za shaba zenye vikalio vya shaba. Lakini kulabu za nguzo hizo na vitanzi vyake vitakuwa vya fedha.