1 Bezaleli alitengeneza sanduku kwa mbao za mjohoro; urefu wake ulikuwa sentimita 110, upana sentimita 66, na kimo chake sentimita 66.
2 Alilipaka dhahabu safi ndani na nje, na kulifanyia ukingo wa dhahabu pande zote.
3 Kisha alitengeneza pete nne za dhahabu za kulibebea, akazitia kwenye pembe zake, kila pembe pete moja.
4 Alitengeneza mipiko ya mjohoro na kuipaka dhahabu.
5 Mipiko hiyo akaipitisha katika zile pete zilizo katika pande mbili za sanduku, kwa ajili ya kulibebea.
6 Alitengeneza kiti cha rehema cha dhahabu safi; urefu wake sentimita 110, na upana wake sentimita 66.
7 Alitengeneza pia viumbe wenye mabawa wawili kwa kufua dhahabu kwenye miisho ya kifuniko hicho;
8 kiumbe kimoja mwisho huu na kingine mwisho mwingine. Alitengeneza viumbe hivyo vyenye mabawa kwenye miisho ya kifuniko hicho, vikiwa kitu kimoja na kifuniko.
9 Viumbe hivyo vilikuwa vimeelekeana, mabawa yao yamekunjuliwa kukifunika kifuniko cha sanduku; nyuso zao zilikielekea kifuniko cha sanduku.
10 Vilevile alitengeneza meza ya mjohoro yenye urefu wa sentimita 88, upana sentimita 44, na kimo chake sentimita 66.
11 Aliipaka dhahabu safi na kuitengenezea ukingo wa dhahabu.
12 Aliizungushia mviringo wa ubao wenye upana wa milimita 75, na kuifanyia ukingo wa dhahabu.
13 Aliitengenezea pete nne za dhahabu na kuzitia katika pembe zake nne mahali miguu ilipoishia.
14 Pete hizo za kushikilia ile mipiko ya kulibebea ziliwekwa karibu na ule mviringo wa ubao.
15 Alitengeneza mipiko miwili ya mjohoro ya kulibebea, akaipaka dhahabu.
16 Alitengeneza vyombo vya dhahabu safi vya kuweka juu ya meza: Sahani zake na visahani kwa ajili ya ubani, na bilauri zake na bakuli kwa ajili ya tambiko za kinywaji.
17 Alitengeneza pia kinara cha taa kwa dhahabu safi. Tako lake, na ufito wa hicho kinara ulikuwa kitu kimoja pamoja na vikombe vyake, matumba yake na maua yake.
18 Matawi sita yalitokeza kila upande wa ufito wake, matawi matatu upande mmoja na matawi matatu upande mwingine.
19 Katika kila tawi kulikuwa na vikombe vitatu mfano wa maua ya mlozi, kila kimoja na tumba lake na ua lake.
20 Na katika ufito kulikuwa na vikombe vinne mfano wa maua ya mlozi, pamoja na matumba yake na maua yake.
21 Mahali pale palipotokezea jozi tatu za matawi chini ya kila jozi kulikuwa na tumba moja.
22 Matumba hayo na matawi vilikuwa kitu kimoja na kinara hicho, na chote kilifuliwa kwa dhahabu safi.
23 Alikitengenezea taa saba, koleo na visahani vyake kwa dhahabu safi.
24 Alikitengeneza kinara hicho na vifaa vyake kwa kilo thelathini na tano za dhahabu.
25 Alitengeneza madhabahu ya kufukizia ubani kwa mbao za mjohoro. Madhabahu hiyo ilikuwa ya mraba, sentimita 45 kwa sentimita 45, na kimo chake sentimita 90. Pembe za madhabahu hiyo zilikuwa kitu kimoja na madhabahu yenyewe.
26 Yote aliipaka dhahabu safi: Upande wake wa juu, pande zake za ubavuni na pembe zake; pia aliitengenezea ukingo wa dhahabu.
27 Alitengeneza pete mbili za dhahabu chini ya ukingo kwenye pande mbili zinazokabiliana. Pete hizo zilitumika kushikilia mipiko ya kuibebea.
28 Alifanya mipiko miwili ya mjohoro na kuipaka dhahabu.
29 Alitengeneza mafuta matakatifu ya kupaka, na ubani safi wenye harufu nzuri uliochanganywa vizuri kama manukato.