1 “Bezaleli na Oholiabu, pamoja na kila mwanamume ambaye Mwenyezi-Mungu amemjalia uwezo na akili ya kujua namna ya kufanya kazi zote katika ujenzi wa hema takatifu, atafanya kazi kulingana na yote ambayo Mwenyezi-Mungu aliamuru.”
2 Mose alimwita Bezaleli na Oholiabu na kila mtu ambaye alikuwa amejaliwa ujuzi na Mwenyezi-Mungu, na kila mtu ambaye moyo wake ulimsukuma kufanya kazi kwa hiari.
3 Hao wakapokea kutoka kwa Mose vitu vyote vilivyotolewa na Waisraeli kwa hiari kwa ajili ya kazi ya hema takatifu. Watu waliendelea kumletea michango yao ya hiari kila asubuhi.
4 Watu wote wenye ujuzi waliokuwa wanafanya kazi za kila namna za kujenga hema la mkutano walitoka, kila mmoja katika kazi yake, wakamwendea
5 Mose na kumwambia, “Watu wameleta vitu vingi zaidi ya vile vinavyohitajiwa kwa kazi aliyotuagiza Mwenyezi-Mungu tuifanye.”
6 Basi, Mose akaagiza: “Mtu yeyote, awe mwanamume au mwanamke, asilete mchango zaidi kwa ajili ya hema takatifu.” Watu wakazuiwa kuleta vitu,
7 maana vile walivyokuwa wameleta vilitosha kwa kazi hiyo na kubaki.
8 Wanaume wote wenye ujuzi walitengeneza hema takatifu kwa mapazia kumi ya kitani safi iliyosokotwa, na kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kuyatarizi viumbe wenye mabawa.
9 Urefu wa kila pazia ulikuwa mita 12 na upana mita 2. Mapazia yote yalikuwa ya kipimo kimoja.
10 Aliyaunga mapazia matano kufanya kipande kimoja na kufanya vivyo hivyo na yale mengine matano.
11 Alitengeneza vitanzi vya buluu upindoni mwa pazia la mwisho la kipande cha kwanza, na vitanzi vingine katika pazia la mwisho la kipande cha pili.
12 Alitia vitanzi hamsini katika pazia la kwanza la kipande cha kwanza, na vitanzi hamsini kwenye utepe wa pazia la pili; vitanzi vyote vilielekeana.
13 Kisha alitengeneza vifungo hamsini vya dhahabu ili kuunganishia vile vipande viwili vya mapazia; hivyo, hema likawa kitu kimoja.
14 Kisha alitengeneza pia kifuniko cha hema kwa mapazia kumi na moja ya manyoya ya mbuzi.
15 Kila pazia lilikuwa na urefu wa mita 13, na upana wa mita 2. Mapazia yote 11 yalikuwa ya kipimo kilekile.
16 Basi, akayaunganisha mapazia matano pamoja, na mapazia sita pamoja.
17 Kisha alifanya vitanzi hamsini upindoni mwa pazia la mwisho la kipande cha kwanza, na vitanzi hamsini upindoni mwa kipande cha pili.
18 Halafu akatengeneza vifungo hamsini vya shaba ili kuunganishia vile vipande viwili vya mapazia, na hivyo kufanya pazia moja la hema.
19 Kisha alitengeneza kifuniko cha ngozi laini ya kondoo dume, na juu yake kifuniko kingine cha ngozi laini ya mbuzi.
20 Halafu akalitengenezea hema mbao za mjohoro za kusimama wima.
21 Kila ubao ulikuwa na urefu wa mita 4 na upana wa sentimita 66.
22 Kila ubao ulikuwa na ndimi mbili za kuunganishia. Mbao zote za hema alizifanyia ndimi.
23 Mbao hizo za hema zilitengenezwa hivi: Mbao ishirini upande wa kusini,
24 na vikalio arubaini vya fedha chini ya hizo mbao 20; vikalio viwili chini ya kila ubao ili kushikilia zile ndimi zake mbili.
25 Na upande wa pili, yaani kaskazini mwa hema, alitengeneza pia mbao ishirini,
26 na vikalio vyake arubaini vya fedha; vikalio viwili chini ya kila ubao.
27 Upande wa nyuma, yaani magharibi mwa hema, alitengeneza mbao sita.
28 Alitengeneza pia mbao mbili kwa ajili ya pembe za hema upande wake wa nyuma.
29 Mbao hizo mbili za pembeni ziliachana chini lakini zilishikamanishwa kwenye pete ya kwanza. Mbao mbili kwa ajili ya hizo pembe mbili zilitengenezwa namna hiyo.
30 Hivyo kulikuwa na mbao nane na vikalio vyake vya fedha kumi na sita, vikalio viwili chini ya kila ubao.
31 Alitengeneza pia pau za mjohoro: Pau tano kwa ajili ya mbao za upande mmoja wa hema,
32 pau tano kwa ajili ya upande wa pili wa hema, na pau tano kwa ajili ya mbao za upande wa nyuma wa hema, ulio magharibi.
33 Alitengeneza upau wa katikati uliofika nusu ya jengo la hema ambao ulipenya katikati kutoka mwisho hadi mwisho.
34 Mbao zote alizipaka dhahabu, akazitengeneza na pete za dhahabu za kushikilia pau hizo ambazo pia alizipaka dhahabu.
35 Alitengeneza pazia la nyuzi za rangi ya buluu, zambarau na nyekundu na kitani safi iliyosokotwa. Pazia hilo lilitariziwa viumbe wenye mabawa kwa ustadi.
36 Alitengeneza nguzo nne za mjohoro, akazipaka dhahabu na kuzitilia kulabu za dhahabu. Vilevile alizifanyia vikalio vinne vya fedha.
37 Kadhalika, kwa ajili ya mlango wa hema, alitengeneza pazia kwa nyuzi za rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa, nalo pazia lilitariziwa vizuri,
38 na nguzo zake tano zikiwa na kulabu. Matumba yake na vifungo vyake alivipaka dhahabu, lakini vikalio vyake vitano vilikuwa vya shaba.