1 Kwa kutumia sufu ya rangi ya buluu, ya zambarau na nyekundu walifuma sare za kuvaa wakati wa kuhudumu mahali patakatifu. Walimshonea Aroni mavazi matakatifu kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.
2 Walitengeneza kizibao kwa nyuzi za dhahabu, kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kwa kitani safi iliyosokotwa.
3 Waliifua dhahabu na kuikata katika nyuzi nyembamba ili kuzifuma pamoja na sufu ya rangi ya buluu, ya zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa kwa ustadi.
4 Kizibao hicho kilivaliwa kwa kamba mbili mabegani zilizoshonewa kwenye ncha zake mbili.
5 Mkanda uliofumwa kwa ustadi juu yake ili kuifungia ulikuwa kitu kimoja na kizibao hicho, na ulitengenezwa kwa vitu hivyohivyo: Dhahabu, sufu ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.
6 Kisha waliandaa vito vya sardoniki na kuvipanga katika vijalizo vya dhahabu; navyo vilichorwa, kama mtu achoravyo mhuri, majina kumi na mawili ya wana wa Israeli.
7 Waliviweka vito hivyo katika kanda za mabegani za kile kizibao ili kuwakilisha makabila kumi na mawili ya Israeli, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.
8 Mafundi walitengeneza kifuko cha kifuani kama vile walivyokitengeneza kile kizibao, kwa dhahabu, kwa sufu ya rangi ya buluu, rangi zambarau na nyekundu, na kwa kitani safi iliyosokotwa.
9 Kifuko hicho kilikuwa cha mraba, sentimita 22 kwa sentimita 22 nacho kilikunjwa.
10 Kifuko hicho kilipambwa kwa safu nne za mawe ya thamani; safu ya kwanza ilikuwa ya akiki, topazi na almasi nyekundu;
11 safu ya pili ilikuwa ya zumaridi, na johari ya rangi ya samawati na almasi;
12 safu ya tatu ilikuwa ya yasintho, ya akiki nyekundu na amethisto;
13 na safu ya nne ilikuwa ya zabarajadi, ya shohamu na yaspi; yote yalimiminiwa vijalizo vya dhahabu.
14 Basi, palikuwa na mawe kumi na mawili yaliyochorwa majina kumi na mawili ya wana wa Israeli. Yalikuwa yamechorwa kama wachoravyo mhuri, kila moja limechorwa jina kuwakilisha makabila kumi na mawili.
15 Walikitengenezea kile kifuko cha kifuani mikufu ya dhahabu safi.
16 Walitengeneza vijalizo viwili vya dhahabu safi na pete mbili za dhahabu, na kuzitia pete hizo kwenye ncha mbili za juu za kifuko hicho.
17 Mikufu hiyo miwili ya dhahabu waliifunga kwenye pete hizo za kifuko cha kifuani.
18 Zile ncha mbili za mikufu ya dhahabu walizitia kwenye vile vijalizo viwili wakazishikamanisha na vile vipande viwili vya mabegani vya kizibao, upande wa mbele.
19 Walitengeneza pete mbili za dhahabu, wakazitia penye ncha mbili za chini upande wa ndani wa kifuko hicho cha kifuani karibu na kizibao.
20 Walitengeneza pete nyingine mbili za dhahabu na kuzitia mbele katika ncha za chini za vipande vya kizibao, mahali kinapoungana na ule mkanda uliofumwa kwa ustadi.
21 Walifunga kifuko cha kifuani kwenye kizibao kwa kufunganisha pete zake na kizibao kwa kamba ya rangi ya buluu, ili kifuko hicho kisilegee ila kikalie ule mkanda uliofumwa kwa ustadi, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.
22 Alitengeneza kanzu ya kuvaa ndani ya kizibao ya rangi ya buluu.
23 Joho hilo lilikuwa na nafasi ya kupitishia kichwa katikati, nayo ilizungushiwa utepe uliofumwa ili isichanike.
24 Kwenye upindo wa chini wa kanzu walifuma mapambo ya makomamanga ya rangi ya buluu, ya zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa.
25 Kisha walitengeneza njuga za dhahabu, na kila baada ya komamanga walitia njuga kwenye upindo wa joho.
26 Hivyo, njuga na komamanga vilifuatana kuuzunguka upindo wa joho hilo, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.
27 Kisha wakawafumia Aroni na wanawe vizibao vya kitani safi,
28 kilemba cha kitani safi, kofia za kitani safi, suruali za kitani safi iliyosokotwa,
29 na mikanda ya kitani safi iliyosokotwa kwa sufu ya rangi ya buluu, ya zambarau na nyekundu na kuitarizi vizuri, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.
30 Kisha walitengeneza pambo la dhahabu safi kwa ajili ya taji takatifu na kuchora juu yake kama wachoravyo mhuri, “Wakfu kwa Mwenyezi-Mungu.”
31 Kisha wakalifunga mbele ya kile kilemba kwa ukanda wa rangi ya buluu, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.
32 Basi, kazi yote ya hema la mkutano ikamalizika. Waisraeli walifanya yote kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.
33 Wakamletea Mose hema takatifu pamoja na vyombo vyake vyote, vikonyo vyake, mbao zake, pau zake, nguzo zake na vikalio vyake;
34 kifuniko cha ngozi za kondoo dume na mbuzi kilichotiwa rangi nyekundu, pazia la mahali patakatifu,
35 sanduku la agano, mipiko yake na kiti cha rehema;
36 meza na vyombo vyake vyote, mikate iliyowekwa mbele ya Mungu;
37 kinara cha taa cha dhahabu safi, taa zake, vyombo vyake vyote pamoja na mafuta kwa ajili ya taa hizo;
38 madhabahu ya dhahabu; mafuta ya kupaka, ubani wenye harufu nzuri, na pazia la mlango wa hema;
39 madhabahu ya shaba na wavu wake wa shaba, mipiko yake na vyombo vyake vyote; bakuli, birika na tako lake;
40 vyandarua vya ua, nguzo zake na vikalio vyake; pazia la mlango wa ua, kamba zake na vigingi vyake; vyombo vyote vilivyohitajika katika huduma ya hema takatifu, yaani hema la mkutano;
41 na mavazi yote yaliyofumwa vizuri kabisa kwa ajili ya huduma ya mahali patakatifu, yaani mavazi matakatifu ya kuhani Aroni, na ya wanawe kwa ajili ya huduma ya ukuhani.
42 Waisraeli walifanya kila kitu kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.
43 Mose alikagua kila kitu, akaridhika kwamba walikuwa wamefanya kila kitu kama Mwenyezi-Mungu alivyoamuru. Hivyo Mose akawabariki.