1 “Utatengeneza madhabahu kwa mbao za mjohoro ili pawe mahali pa kufukizia ubani.
2 Madhabahu hiyo iwe ya mraba, urefu na upana wake sentimita 45, na kimo chake sentimita 90. Pembe zake za juu zitatokeza zote zikiwa kitu kimoja na madhabahu yenyewe.
3 Yote utaipaka dhahabu safi: Upande wake wa juu, pande zake zote za ubavuni na pembe zake; pia utaizungushia ukingo wa dhahabu.
4 Utaitengenezea pete mbili za dhahabu na kuzitia chini ya ukingo wake kwenye pande mbili zinazokabiliana; hizo pete zitatumiwa kushikilia mipiko wakati wa kuibeba.
5 Mipiko hiyo iwe ya mjohoro na ipakwe dhahabu.
6 Madhabahu hiyo iwekwe mbele ya pazia kando ya sanduku la maamuzi, mbele ya kiti cha huruma ambapo nitakutana nawe.
7 Kila siku Aroni anapoingia kuzitayarisha taa zilizopo hapo, atafukiza ubani wenye harufu nzuri juu ya madhabahu hiyo.
8 Tena atafukiza ubani wakati wa jioni anapowasha taa. Tambiko hii ya ubani itatolewa daima bila kukatizwa katika vizazi vyenu vyote.
9 Kwenye madhabahu hiyo, kamwe msifukize ubani usio mtakatifu, wala msitoe sadaka ya kuteketezwa, wala sadaka ya nafaka, wala kumimina juu yake sadaka ya kinywaji.
10 Aroni hana budi kufanya upatanisho juu ya pembe za madhabahu hiyo mara moja kwa mwaka. Ataifanyia upatanisho kwa damu ya tambiko ya kuondolea dhambi mara moja kila mwaka katika vizazi vyenu vyote maana madhabahu hiyo ni takatifu kabisa kwangu mimi Mwenyezi-Mungu.”
11 Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose,
12 “Kila utakapowahesabu Waisraeli, kila mmoja atalipa fidia kwa ajili ya nafsi yake mbele yangu ili pasiwe na maradhi mabaya miongoni mwao wakati wa kuhesabiwa.
13 Kila mmoja atakayehesabiwa ni lazima alipe kiasi cha fedha kulingana na vipimo vya hema la mkutano. Hii ni sadaka yake atakayonitolea.
14 Kila mmoja atakayehesabiwa, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, atanitolea tambiko hiyo.
15 Tajiri asitoe zaidi wala maskini asitoe chini ya nusu ya kiasi hicho cha fedha wakati mnaponitolea sadaka hiyo ili kufanya upatanisho.
16 Wewe utaipokea fedha hiyo ya upatanisho kutoka kwa Waisraeli, nawe utaitumia kwa shughuli za kazi za hema takatifu, nayo iwe ni ukumbusho wa Waisraeli mbele yangu, fidia ya maisha yenu.”
17 Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose,
18 “Utatengeneza birika la shaba la kutawadhia lenye tako la shaba, uliweke katikati ya hema la mkutano na madhabahu, na kutia maji ndani yake.
19 Aroni na wanawe watatumia maji hayo kunawia mikono na miguu,
20 kabla ya kuingia kwenye hema la mkutano au kukaribia madhabahu ili kunitolea tambiko mimi Mwenyezi-Mungu, tambiko zitolewazo kwa moto; watafanya hivyo wasije wakafa.
21 Ni lazima wanawe mikono na miguu yao wasije wakafa. Hii itakuwa ni kanuni kwao daima, tangu Aroni na uzao wake, vizazi hata vizazi.”
22 Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose,
23 “Utachukua viungo bora kabisa kama vifuatavyo: Manemane ya maji kilo sita, mdalasini wenye harufu nzuri kilo tatu, miwa yenye harufu nzuri kilo tatu,
24 na aina nyingine ya mdalasini kilo 6 – vipimo hivyo vyote viwe kufuatana na vipimo vya hema takatifu; chukua pia lita 4 za mafuta.
25 Kutokana na viungo hivyo utatengeneza mafuta matakatifu uyachanganye kama afanyavyo fundi wa manukato; hayo yatatumika kuweka vitu wakfu.
26 Kisha utalimiminia mafuta hayo hema la mkutano, na sanduku la maamuzi;
27 meza na vyombo vyake vyote; kinara cha taa na vyombo vyake, madhabahu ya kufukizia ubani,
28 madhabahu ya sadaka za kuteketezwa na vyombo vyake vyote, birika na tako lake.
29 Utaviweka wakfu, ili viwe vitakatifu kabisa. Chochote kitakachovigusa vifaa hivyo, kitakuwa kitakatifu.
30 Kisha mpake mafuta Aroni na wanawe na kuwaweka wakfu ili wanitumikie kama makuhani.
31 Waambie Waisraeli kwamba haya yatakuwa mafuta yangu matakatifu ya kupaka katika vizazi vyenu vyote.
32 Mafuta haya kamwe yasimiminiwe mtu yeyote wa kawaida, wala yasitengenezwe mafuta mengine ya aina hii; haya ni mafuta matakatifu na ni lazima yawe daima matakatifu kwenu.
33 Yeyote atakayetengeneza mafuta kama haya, au kumpaka mtu asiyestahili kupakwa mafuta haya, mtu huyo atatengwa mbali na watu wake.”
34 Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Utachukua vipimo vinavyolingana vya viungo vitamu vifuatavyo: Utomvu wa natafi, utomvu wa shekelethi, utomvu wa kelbena na ubani safi.
35 Utatumia vitu hivyo kutengenezea ubani kama utengenezwavyo na fundi manukato, utiwe chumvi upate kuwa safi na mtakatifu.
36 Kisha utasagwa na kufanya unga laini, upate kutumiwa ndani ya hema la mkutano na kulipaka sanduku la agano, mahali nitakapokutana nawe; huo utakuwa ubani mtakatifu kabisa kwenu.
37 Kamwe msifanye ubani wa mchanganyiko huo kwa matumizi yenu wenyewe kwani ubani huo utakuwa mtakatifu mbele yangu.
38 Yeyote atakayejitengenezea ubani wa aina hiyo na kuutumia kama manukato yake binafsi, atatengwa mbali na watu wake.”