1 Mose alikusanya jumuiya yote ya Waisraeli, akawaambia, “Haya ndiyo mambo ambayo Mwenyezi-Mungu amewaamuru muyafanye:
2 Kwa siku sita mtafanya kazi zenu; lakini siku ya saba ni Sabato siku ya mapumziko ambayo ni wakfu kwa Mwenyezi-Mungu. Yeyote atakayefanya kazi siku hiyo lazima auawe.
3 Msiwashe hata moto katika makao yenu siku ya Sabato.”
4 Mose aliiambia jumuiya yote ya Waisraeli, “Hili ndilo jambo ambalo Mwenyezi-Mungu amewaamuru mlifanye:
5 Mtatoa katika mali zenu mchango wa kumpa Mwenyezi-Mungu. Kila mtu mwenye moyo mwema atamletea Mwenyezi-Mungu mchango: Dhahabu, fedha, shaba;
6 sufu ya buluu, ya zambarau na nyekundu; kitani safi iliyosokotwa; manyoya ya mbuzi;
7 ngozi za kondoo dume zilizotiwa rangi nyekundu, ngozi za mbuzi; mbao za mjohoro,
8 mafuta kwa ajili ya taa, viungo kwa ajili ya mafuta ya kupaka na kwa ajili ya ubani wenye harufu nzuri;
9 vito vya sardoniki na vito vingine kwa ajili ya mapambo ya kizibao na kifuko cha kifuani.
10 “Kila mtu mwenye ujuzi wa kazi fulani miongoni mwenu atakuja kufanya vitu vyote alivyoamuru Mwenyezi-Mungu:
11 Kutengeneza hema takatifu, kifuniko chake na pazia lake, kulabu zake, pau zake, vikalio vyake;
12 sanduku la agano pamoja na mipiko yake, kiti cha rehema, pazia la mahali patakatifu sana;
13 meza na mipiko yake pamoja na vyombo vyake vyote, mikate iliyowekwa mbele ya Mwenyezi-Mungu;
14 vinara vya taa pamoja na vyombo vyake vyote, taa zake na mafuta yake;
15 madhabahu ya ubani na mipiko yake, mafuta ya kupaka na ubani wenye harufu nzuri, pazia la mlango wa hema takatifu;
16 madhabahu ya sadaka za kuteketezwa pamoja na wavu wa shaba, mipiko yake pamoja na vyombo vyake vyote, birika na tako lake;
17 vyandarua vya ua, nguzo zake na vikalio vyake, pazia la mlango wa ua;
18 vigingi vya hema takatifu na vya ua pamoja na kamba zake;
19 mavazi yaliyofumwa vizuri kabisa kwa ajili ya huduma ya mahali patakatifu, yaani mavazi matakatifu ya kuhani Aroni na ya wanawe, kwa ajili ya huduma yao ya ukuhani.”
20 Basi, jumuiya yote ya Waisraeli ikaondoka mbele ya Mose.
21 Kila mtu aliyevutwa na kusukumwa moyoni mwake alimtolea Mungu mchango wake kwa ajili ya hema la mkutano, huduma zake zote na mavazi yake matakatifu.
22 Hivyo wote wenye moyo mkarimu, wanaume kwa wanawake, wakaleta vipini, pete za mhuri, vikuku na kila aina ya vyombo vya dhahabu; kila mtu akamtolea Mwenyezi-Mungu kitu cha dhahabu.
23 Kila mtu alileta chochote alichokuwa nacho kama vile sufu ya rangi ya buluu zambarau na nyekundu, au kitani safi, au manyoya ya mbuzi au ngozi ya kondoo iliyotiwa rangi nyekundu.
24 Kila mtu aliyeweza kutoa fedha au shaba aliileta kwa Mwenyezi-Mungu kama toleo lake. Tena mtu yeyote aliyekuwa na mbao za mjohoro alileta pia.
25 Wanawake wote waliokuwa na ujuzi wa kufuma walileta vitu walivyofuma kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu na kitani safi iliyosokotwa.
26 Na wanawake wote waliokuwa na ujuzi walisokota manyoya ya mbuzi.
27 Viongozi walileta vito vya rangi na mawe mengine kwa ajili ya kizibao na kifuko cha kifuani;
28 walileta pia viungo na mafuta kwa ajili ya taa, mafuta ya kupaka na ubani wenye harufu nzuri.
29 Waisraeli wote, wanaume kwa wanawake, ambao walivutwa moyoni mwao kuleta chochote kwa ajili ya kazi ambayo Mwenyezi-Mungu alikuwa amemwagiza Mose ifanyike, walileta vitu hivyo kwa hiari, kama mchango wa kumpa Mwenyezi-Mungu.
30 Mose aliwaambia Waisraeli; “Tazameni! Mwenyezi-Mungu amemteua Bezaleli, mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda.
31 Amemjaza roho yake, amempa ujuzi, akili, maarifa na ufundi,
32 abuni michoro ya sanaa na kufanya kazi za kufua dhahabu, fedha na shaba;
33 achonge mawe ya kupambia na mbao kwa ajili ya kazi nyingine zote za kifundi.
34 Pia amemwongoza yeye na Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani wawafundishe wengine.
35 Amewapa ujuzi wa kufanya kila kazi ya ufundi au ifanywayo na watu wa sanaa au mafundi wa kutarizi kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu na kitani safi iliyosokotwa, kwa kutumia ufundi wowote wa msanii.