1 Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose na Aroni, walipokuwa bado nchini Misri,
2 “Mwezi huu utakuwa kwenu mwezi wa kwanza wa mwaka.
3 Iambieni jumuiya yote ya Waisraeli kwamba mnamo siku ya kumi ya mwezi huu, mtachukua mwanakondoo mmoja kwa kila jamaa moja.
4 Kama jamaa moja ni ndogo mno hata isiweze kumaliza kondoo mmoja, itashirikiana na jamaa jirani kadiri ya idadi ya watu wake; kisha watachagua mnyama ambaye kila mtu ataweza kula.
5 Mwanakondoo huyo asiwe na kilema chochote, awe wa kiume na wa mwaka mmoja. Anaweza kuwa mwanakondoo au mwanambuzi.
6 Mtamweka mnyama huyo mpaka siku ya kumi na nne ya mwezi huu. Siku hiyo, jumuiya yote ya Waisraeli watawachinja wanyama hao wakati wa jioni.
7 Kisha, watachukua damu ya hao wanyama na kupaka kwenye miimo na vizingiti vya kila nyumba watakamolia wanyama hao.
8 Wataila nyama hiyo usiku huohuo baada ya kuichoma; wataila pamoja na mkate usiotiwa chachu na mboga chungu za majani.
9 Imekatazwa kuila ikiwa mbichi au imechemshwa kwa maji, bali lazima ichomwe yote, pamoja na kichwa, miguu na nyama zake za ndani.
10 Hali kadhalika msibakize nyama yoyote mpaka asubuhi. Nyama yoyote itakayobaki hadi asubuhi mtaiteketeza motoni.
11 Na hivi ndivyo mtakavyomla mnyama huyo: Mtakuwa mmejifunga mikanda viunoni mwenu, mmevaa viatu na fimbo zenu mikononi. Tena mtamla kwa haraka. Hiyo ni Pasaka ya Mwenyezi-Mungu.
12 “Usiku huo, nitapita katika nchi ya Misri na kuwaua wazaliwa wa kwanza wa Misri, watu kwa wanyama. Nitaiadhibu miungu yote ya Misri. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.
13 Basi, ile damu itakuwa ishara yenu ya kuonesha nyumba mtakamokuwa. Nami nitakapoiona hiyo damu, nitawapita nyinyi, na hamtapatwa na dhara lolote wakati nitakapoipiga nchi ya Misri.
14 Vizazi hata vizazi mtaadhimisha tukio hilo kwa sikukuu kubwa kwa heshima yangu mimi Mwenyezi-Mungu. Hilo litakuwa agizo la milele kwenu.”
15 Mwenyezi-Mungu akasema, “Kwa muda wa siku saba, mtakula mikate isiyotiwa chachu. Siku ya kwanza ya siku hizo saba, mtaondoa chachu katika nyumba zenu. Mtu yeyote akila kitu kilichotiwa chachu katika muda huo wa siku saba, ni lazima aondolewe miongoni mwa Waisraeli.
16 Siku ya kwanza na siku ya saba mtakuwa na mkutano mtakatifu. Katika siku hizo mbili hamtaruhusiwa kufanya kazi yoyote isipokuwa kazi ya lazima ya kutayarisha chakula.
17 Mtaadhimisha sikukuu hii ya mikate isiyotiwa chachu kama ukumbusho wa siku nilipowatoa nyinyi, vikundi vya Israeli, kutoka Misri. Sikukuu hiyo itaadhimishwa na vizazi vyenu vyote vijavyo, kama agizo la milele.
18 Basi, mtakula mikate isiyotiwa chachu kuanzia jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza, mpaka jioni ya siku ya ishirini na moja ya mwezi huohuo wa kwanza.
19 Katika siku hizo saba, msiwe na chachu yoyote katika nyumba zenu. Mtu yeyote, awe mgeni au mwenyeji, akila kitu kilichotiwa chachu, ataondolewa miongoni mwa jumuiya ya Waisraeli.
20 Popote pale mnapoishi, ni mwiko kabisa kula chochote kilichotiwa chachu. Mnapaswa kula mikate isiyotiwa chachu.”
21 Basi, Mose akawaita wazee wote wa Waisraeli, akawaambia, “Chagueni kila mmoja wenu, kulingana na jamaa yake, mwanakondoo na kumchinja kwa sikukuu ya Pasaka.
22 Mtachukua majani ya husopo na kuyachovya katika damu ndani ya birika na kupaka kwenye vizingiti na miimo yote miwili ya milango ya nyumba zenu. Mtu yeyote asitoke nje ya nyumba usiku huo hadi asubuhi.
23 Maana mimi Mwenyezi-Mungu nitapita kuwaua Wamisri. Lakini nitakapoiona damu iliyopakwa kwenye vizingiti na miimo ya nyumba zenu, nitazipita na wala sitamruhusu mwangamizi kuingia katika nyumba zenu na kuwaua.
24 Shikeni jambo hilo nyinyi na wazawa wenu kama agizo la milele.
25 Mtakapoingia katika nchi ile ambayo mimi Mwenyezi-Mungu nitawapa, kama nilivyoahidi, ni lazima kulitekeleza.
26 Kila wakati watoto wenu watakapowauliza, ‘Jambo hili lina maana gani?’
27 Nyinyi mtawajibu, ‘Hii ni tambiko ya Pasaka kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu, kwa sababu alizipita nyumba za Waisraeli nchini Misri alipowaua Wamisri, lakini sisi hakutuua.’” Waisraeli wakainamisha vichwa na kumwabudu Mwenyezi-Mungu.
28 Kisha Waisraeli wakaenda, wakafanya kama walivyoambiwa na Mose na Aroni kulingana na amri ya Mwenyezi-Mungu.
29 Mnamo usiku wa manane, Mwenyezi-Mungu aliwaua wazaliwa wa kwanza wote wa Misri. Wote walikufa, tangu mzaliwa wa kwanza wa Farao, mrithi wa ufalme, hadi mzaliwa wa kwanza wa mfungwa gerezani. Hata wazaliwa wa kwanza wa wanyama nao walikufa.
30 Basi Farao, watumishi wake na wakazi wote wa Misri wakaamka usiku. Kukawa na kilio kikubwa nchini kote Misri kwa maana hapakuwa hata nyumba moja ambamo hakufa mtu.
31 Hapo Farao akawaita Mose na Aroni, usiku huohuo, akamwambia, “Amkeni! Ondokeni miongoni mwa watu wangu. Nendeni, nyinyi pamoja na hao Waisraeli, mkamtumikie Mwenyezi-Mungu kama mlivyosema.
32 Chukueni makundi yenu ya kondoo na ng'ombe, mwondoke; niombeeni na mimi baraka.”
33 Wamisri wakawahimiza Waisraeli waondoke haraka, wakisema, “Hakika tutakufa sote!”
34 Basi, Waisraeli wakauchukua unga wao uliokandwa kabla haujatiwa chachu, na mabakuli yao ya kukandia wakiwa wamezifunga kwa nguo na kubeba mabegani.
35 Waisraeli walikuwa wamekwisha fanya kama Mose alivyowaagiza hapo awali: Waliwaomba Wamisri wawapatie vito vya fedha, dhahabu na mavazi.
36 Naye Mwenyezi-Mungu alikwisha wafanya Waisraeli wapendwe na Wamisri, nao Wamisri wakawapa kila kitu walichoomba. Ndivyo Waisraeli walivyowapokonya Wamisri mali yao.
37 Waisraeli waliondoka mjini Ramesesi, wakasafiri kwa miguu kuelekea Sukothi. Walikuwa wanaume wapatao 600,000, licha ya wanawake na watoto.
38 Kulikuwa pia na kundi la watu wengine walioandamana nao pamoja na mifugo mingi, kondoo na ng'ombe.
39 Kwa kuwa walikuwa wameondoka Misri kwa haraka, hawakuweza kutayarisha chakula cha safarini, ila tu ule unga uliokandwa bila kutiwa chachu. Basi, wakaoka mikate isiyotiwa chachu.
40 Waisraeli walikuwa wameishi nchini Misri kwa muda wa miaka 430.
41 Katika siku ya mwisho ya mwaka wa 430, siku hiyohiyo maalumu ndipo makabila yote ya Mwenyezi-Mungu yaliondoka nchini Misri.
42 Usiku huo ambao Mwenyezi-Mungu alikesha ili kuwatoa Waisraeli nchini Misri, unapaswa kuadhimishwa na Waisraeli wote na vizazi vyao vyote, kama usiku wa kukesha kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu.
43 Mwenyezi-Mungu aliwaambia Mose na Aroni, “Yafuatayo ni maagizo juu ya adhimisho la Pasaka. Mgeni yeyote hatashiriki chakula cha Pasaka.
44 Lakini mtumwa yeyote aliyenunuliwa kwa fedha, baada ya kumtahiri, ataruhusiwa kushiriki.
45 Msafiri yeyote, wala kibarua yeyote, hatashiriki chakula hicho.
46 Mwanakondoo wa Pasaka ataliwa katika nyumba moja. Hamtatoa nyama yoyote nje ya nyumba alimochinjiwa, wala hamtavunja hata mfupa mmoja wa mnyama wa Pasaka.
47 Jumuiya yote ya watu wa Israeli itaadhimisha sikukuu hiyo.
48 Mgeni yeyote anayeishi miongoni mwenu akipenda kuadhimisha sikukuu ya Pasaka, ni lazima kwanza wanaume wote wa nyumba yake watahiriwe; hapo atahesabiwa kuwa kama mwenyeji na kuruhusiwa kushiriki. Mwanamume yeyote asiyetahiriwa asishiriki kamwe.
49 Sheria zilezile zitamhusu mzalendo Mwisraeli na wageni watakaoishi miongoni mwenu”.
50 Waisraeli wote walitii sheria hiyo na kufanya kama Mwenyezi-Mungu alivyowaagiza Mose na Aroni.
51 Siku hiyohiyo Mwenyezi-Mungu aliwatoa Waisraeli nchini Misri kwa makundi.