11 Leo hii na muwarudishie mashamba yao, mashamba ya mizabibu, mashamba ya mizeituni na nyumba zao, hata na riba ya fedha, nafaka, divai, na mafuta ambayo nilikuwa ninawatoza.”
12 Wao wakaitikia na kusema, “Tutawarudishia na hatutawadai chochote. Tutafanya kama ulivyosema.” Nikawaita makuhani mbele, na viongozi wote wakaapa mbele ya makuhani kufanya kama walivyoahidi.
13 Nilikunguta kibindo changu na kusema, “Kila mmoja asiyetimiza ahadi hii Mungu na amkungute, amtoe katika nyumba yake na katika kazi yake. Basi, akungutike na kubaki mikono mitupu.” Mkutano mzima ukaitikia, na kusema, “Amina” wakamsifu Mwenyezi-Mungu. Watu wakafanya kama walivyokuwa wameahidi.
14 Tangu wakati nilipoteuliwa kuwa mtawala wa nchi ya Yuda kwa miaka kumi na miwili yaani tangu mwaka wa ishirini mpaka mwaka wa thelathini na mbili wa kutawala kwa mfalme Artashasta, sikula chakula kinachostahili kuliwa na mtawala, wala ndugu zangu hawakufanya hivyo.
15 Watawala walionitangulia walikuwa mzigo mzito kwa watu wakiwadai chakula na divai, mbali na kuwadai kuwalipa sarafu za uzito wa shekeli arubaini za fedha. Hata watumishi wao waliwadhulumu watu. Bali, mimi sikufanya hivyo, kwani nilimcha Mungu.
16 Nilikuwa na juhudi nyingi katika ujenzi mpya wa ukuta huu na kamwe sikujipatia hata shamba. Hata watumishi wangu wote walifanya kazi hii kwa bidii.
17 Zaidi ya hayo, kila siku niliwalisha watu 150, wakiwamo Wayahudi na maofisa, mbali na wale watu waliotujia toka mataifa jirani.