11 Kutoka huko watu wa kabila la Yuda walikwenda kuushambulia mji wa Debiri; ambao hapo awali uliitwa Kiriath-seferi.
12 Kalebu akatangaza: “Mtu yeyote atakayefaulu kuuteka mji wa Kiriath-seferi, nitamwoza binti yangu Aksa.”
13 Basi, Othnieli, mwana wa Kenazi na mdogo wake Kalebu, akauteka, naye Kalebu akamtoa bintiye Aksa aolewe na Othnieli.
14 Aksa alipowasili kwa Othnieli, akamwambia Othnieli amwombe Kalebu baba yake shamba. Aksa alikuwa amepanda punda na aliposhuka chini baba yake alimwuliza, “Ungependa nikupe nini?”
15 Akamjibu, “Nipe zawadi! Naomba unipe chemchemi za maji kwani eneo ulilonipa huko Negebu ni kavu.” Kalebu akampa chemchemi za juu na za chini.
16 Wazawa wa Keni ambaye alikuwa baba mkwe wa Mose, walifuatana na watu wa kabila la Yuda kutoka Mji wa Mitende yaani mji wa Yeriko, mpaka jangwa la Yuda karibu na Aradi, wakafanya makao yao huko pamoja na watu wa Yuda.
17 Watu wa kabila la Yuda walishirikiana na ndugu zao, watu wa kabila la Simeoni, wakawashinda Wakanaani waliokaa Sefathi. Waliuangamiza kabisa mji huo na kugeuza jina lake kuwa Horma.