18 Watu wa kabila la Yuda pia waliteka miji ya Gaza na eneo lake, Ashkeloni na eneo lake, na Ekroni na eneo lake.
19 Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na watu wa kabila la Yuda, nao wakaiteka nchi ya milima. Lakini hawakuweza kuwashinda wenyeji wa nchi tambarare kwa sababu magari yao ya vita yalikuwa ya chuma.
20 Mji wa Hebroni ukakabidhiwa kwa Kalebu kufuatana na maagizo ya Mose. Kalebu akazifukuza kutoka huko koo tatu za Anaki.
21 Lakini watu wa kabila la Benyamini hawakuwafukuza Wayebusi waliokaa mjini Yerusalemu; ndiyo maana Wayebusi wanakaa pamoja na watu wa kabila la Benyamini mjini Yerusalemu mpaka leo.
22 Watu wa makabila ya Yosefu waliushambulia mji wa Betheli, naye Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja nao.
23 Kwanza walikuwa wamewatuma wapelelezi kwenda kuupeleleza mji wa Betheli. Mji huo hapo awali uliitwa Luzu.
24 Wapelelezi hao walimwona mtu mmoja akitoka mjini, wakamwambia, “Tafadhali, tuoneshe njia inayoingia mjini, nasi tutakutendea kwa wema.”