20 Lakini Sihoni hakuwakubali Waisraeli wapite katika nchi yake. Basi, Sihoni akakusanya watu wake wote, akapiga kambi huko Yahasa, akawashambulia Waisraeli.
21 Naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, akamtia Sihoni pamoja na watu wake mikononi mwa Waisraeli, wakawashinda. Hivyo Waisraeli wakachukua nchi yote ya Waamori ambao walikuwa wanaishi huko.
22 Walilichukua eneo lote la Waamori tangu mto Arnoni hadi mto Yaboki na tangu jangwani upande wa mashariki hadi mto Yordani magharibi.
23 Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, akawafukuza Waamori mbele ya Waisraeli. Je, wewe unataka kutunyanganya nchi yetu?
24 Tosheka na kile ambacho mungu wako Kemoshi amekupa. Lakini nchi yoyote ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, amewafukuza wakazi wake, akatupa sisi, hiyo ni mali yetu sisi.
25 Je, unadhani wewe una nguvu kuliko Balaki mwana wa Zipora aliyekuwa mfalme wa Moabu? Yeye hakushindana na Waisraeli au kupigana nao.
26 Wakati wote Waisraeli walipoishi mjini Heshboni na vijiji vyake, na mji wa Aroeri na vijiji vyake pamoja na miji yote iliyo ukingoni mwa mto Arnoni kwa muda wa miaka 300, kwa nini hukulikomboa eneo hilo wakati huo?