3 Siku moja, malaika wa Mwenyezi-Mungu akamtokea huyo mwanamke, akamwambia, “Wewe ni tasa, huna watoto. Lakini utapata mimba na kumzaa mtoto wa kiume.
4 Kwa hiyo uwe mwangalifu, usinywe divai au kileo wala usile kitu chochote kilicho najisi,
5 kwa maana utachukua mimba na kuzaa mtoto wa kiume. Nywele za mtoto huyo kamwe zisinyolewe, maana atakuwa amewekwa wakfu kwa Mungu tangu kuzaliwa kwake. Naye ataanza kuwakomboa Waisraeli mikononi mwa Wafilisti.”
6 Mwanamke huyo akaenda kumwambia mume wake, “Mtu wa Mungu ambaye sura yake ilikuwa kama ya malaika wa Mungu alinijia. Sikumwuliza alikotoka wala hakuniambia jina lake.
7 Lakini aliniambia kwamba nitachukua mimba na kuzaa mtoto wa kiume. Aliniamuru nisinywe divai au kileo wala kula chochote kilicho najisi, maana mtoto huyo atakuwa amewekwa wakfu kwa Mungu tangu kuzaliwa kwake mpaka atakapokufa.”
8 Kisha Manoa akamwomba Mwenyezi-Mungu, akisema, “Nakuomba ee Mwenyezi-Mungu, umtume tena yule mtu wako uliyemtuma ili atufundishe mambo tunayopaswa kumtendea huyo mtoto atakayezaliwa.”
9 Mwenyezi-Mungu akalisikia ombi la Manoa, na yule malaika wa Mungu akamwendea tena yule mwanamke alipokuwa ameketi shambani. Lakini mumewe, Manoa, hakuwa pamoja naye.