12 Waisraeli walitenda tena uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu akampa nguvu mfalme Egloni wa Moabu awashambulie Waisraeli, kwa sababu walitenda uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu.
13 Egloni akawakusanya Waamoni na Waamaleki, akaenda kupigana na Waisraeli, akawashinda. Akauteka Mji wa Mitende yaani Yeriko.
14 Waisraeli wakamtumikia Egloni mfalme wa Moabu, kwa muda wa miaka kumi na minane.
15 Lakini Waisraeli walipomlilia Mwenyezi-Mungu, yeye aliwapelekea mtu wa kuwakomboa, yaani Ehudi mwana wa Gera, mwenye mkono wa shoto, wa kabila la Benyamini.Waisraeli walimtuma apeleke zawadi zao kwa Egloni mfalme wa Moabu.
16 Ehudi akajitengenezea upanga wenye makali kuwili; urefu wake sentimita hamsini. Akaufunga kiunoni mwake upande wa kulia ndani ya mavazi yake.
17 Kisha akampelekea Egloni zile zawadi. Egloni alikuwa mtu mnene sana.
18 Ehudi alipomaliza kutoa zawadi, akawaambia watu waliobeba zawadi, waondoke.