20 Makundi yote matatu kwa pamoja yakapiga tarumbeta na kuvunja magudulia yao. Katika mikono yao ya kushoto walishika mienge na kwa mikono yao ya kulia tarumbeta na kuzipiga, huku wakisema kwa sauti kubwa, “Upanga kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu na kwa ajili ya Gideoni!”
21 Wakasimama kila mmoja mahali pake kuizunguka kambi. Jeshi lote la adui likatawanyika huku likipiga mayowe.
22 Watu wa Gideoni walipopiga tarumbeta zao 300, Mwenyezi-Mungu aliwafanya Wamidiani waanze kuuana wao kwa wao kambini. Waliosalia wakatoroka hadi Serera panapoelekea Beth-shita, hadi mpakani mwa Abel-mehola karibu na Tabathi.
23 Waisraeli wa kabila la Naftali, Asheri, na Manase, wote waliitwa, wakawafuatia Wamidiani.
24 Gideoni akatuma wajumbe kote katika nchi ya milima ya Efraimu watangaze: “Teremkeni kuwakabili Wamidiani na kuwazuia kwa kuteka vijito na mto Yordani mpaka Beth-bara.” Basi, wanaume wote wa Efraimu wakaja na kuuteka mto Yordani mpaka Beth-bara.
25 Wakachukua mateka viongozi wawili wa Midiani, yaani Orebu na Zeebu. Wakamuua Orebu katika mwamba wa Orebu, naye Zeebu wakamuua katika shinikizo la Zeebu, wakiwa wanawafuatia Wamidiani. Wakamletea Gideoni vichwa vya Orebu na Zeebu, ngambo ya mto Yordani.