44 Abimeleki na kundi lake wakaenda mbio kwenda kulinda lango la mji. Makundi yake mawili mengine yaliwashambulia wale waliokuwa mashambani na kuwaua.
45 Abimeleki alipigana na wakazi wa mji huo siku nzima. Akauteka mji na kuwaua watu wote waliokuwamo humo. Akauteketeza mji kwa moto na kuutia chumvi.
46 Watu wote waliokuwa katika mnara wa Shekemu waliposikia habari hizo, walikimbilia kwenye ngome ya nyumba ya mungu aliyeitwa El-berithi.
47 Abimeleki akaambiwa kuwa watu wote waliokuwa kwenye mnara wa Shekemu wamejikusanya pamoja.
48 Abimeleki na watu wake wakaenda mlimani Salmoni, akachukua shoka akakata tawi la mti na kuliweka begani mwake. Halafu akawaambia wale watu aliokuwa nao waharakishe kufanya kama alivyofanya.
49 Kila mmoja akakata tawi kama lile la Abimeleki. Wakachukua matawi yao na kuyaegemeza kwenye kuta za ngome, wakayatia moto na kuichoma ngome; watu wote wanaume na wanawake wapatao 1,000 waliokuwa katika mnara wa Shekemu wakafa.
50 Kisha Abimeleki akaenda Thebesi, akauzingira na kuuteka.