3 Hapo, Mose akamwambia Aroni, “Kwa tukio hili Mwenyezi-Mungu amekuonesha maana ya kile alichosema: ‘Nitajionesha kuwa mtakatifu miongoni mwa wale walio karibu nami; nitatukuzwa mbele ya watu wote!’” Aroni akanyamaza kimya.
4 Basi, Mose akawaita Mishaeli na Elsafani, wanawe Uzieli, baba mdogo wa Aroni, akawaambia waje kuondoa maiti za ndugu zao maskani na kuzipeleka nje ya kambi.
5 Wakachukua maiti za ndugu zao na kuzipeleka nje ya kambi wakiwa wamevaa mavazi yao, kama Mose alivyoamuru.
6 Kisha Mose akamwambia Aroni na wanawe, Eleazari na Ithamari, “Msivuruge nywele zenu na wala msirarue mavazi yenu kuomboleza, la sivyo mtakufa na kuiletea jumuiya yote ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu. Lakini ndugu zenu yaani jumuiya yote ya Israeli, wanaweza kuomboleza kwa sababu ya moto huo aliouleta Mwenyezi-Mungu.
7 Msitoke nje ya mlango wa hema la mkutano, la sivyo mtakufa; kwani mafuta ya kupaka ya Mwenyezi-Mungu yangali juu yenu.” Aroni na wanawe wakafanya kama Mose alivyosema.
8 Mwenyezi-Mungu aliongea na Aroni, akasema,
9 “Mnapoingia ndani ya hema la mkutano, wewe na wanao msinywe divai wala kileo chochote, la sivyo mtakufa. Hii itakuwa sheria ya kudumu katika vizazi vyenu vyote.