19 Kuhani atatolea sadaka ya kuondoa dhambi na kumfanyia huyo mtu anayetakaswa ibada ya upatanisho ili kumwondolea unajisi wake. Kisha atamchinja mwanakondoo wa sadaka ya kuteketezwa.
20 Kuhani atatolea ile sadaka ya kuteketezwa na sadaka ya nafaka juu ya madhabahu. Hivyo kuhani atamfanyia huyo mtu ibada ya upatanisho, naye atakuwa safi.
21 “Lakini ikiwa mtu huyo ni maskini, hana uwezo wa kutoa vitu hivyo, basi ataleta mwanakondoo dume mmoja kuwa fidia ya sadaka ya kuondoa hatia ambaye atafanyiwa ishara ya kutoa sadaka ili kumfanyia huyo mtu ibada ya upatanisho. Ataleta pia kilo moja ya unga laini uliochanganywa na mafuta kwa ajili ya sadaka ya nafaka na mafuta theluthi moja ya lita.
22 Ataleta pia hua wawili au makinda mawili ya njiwa kadiri anavyoweza mmoja atakuwa kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi na mwingine kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa.
23 Siku ya nane atamletea kuhani vitu hivyo mbele ya mlango wa hema la mkutano kwa ajili ya utakaso wake mbele ya Mwenyezi-Mungu.
24 Kuhani atamchukua huyo mwanakondoo dume wa sadaka ya kuondoa hatia pamoja na yale mafuta theluthi moja ya lita na kufanya ishara ya kuvitolea mbele ya Mwenyezi-Mungu.
25 Atamchinja huyo mwanakondoo dume wa sadaka ya kuondoa hatia. Kuhani atachukua kiasi cha damu na kumpaka huyo mtu anayetakaswa katika ncha ya sikio lake la kulia, katika kidole gumba cha mkono wake wa kulia na kidole gumba cha mguu wake wa kulia.