4 basi, kuhani ataamuru watu walete ndege wawili safi walio hai, kipande cha mwerezi, sufu ya rangi nyekundu na tawi la husopo kwa ajili ya huyo mtu atakayetakaswa.
5 Kuhani atawaamuru wamchinje ndege mmoja katika chungu chenye maji safi ya chemchemi.
6 Kuhani atamchukua yule ndege mwingine hai, kipande kile cha mwerezi, sufu ya rangi nyekundu na lile tawi la husopo na kuvitumbukiza vyote katika damu ya yule ndege aliyechinjwa.
7 Kisha, atamnyunyizia huyo mwenye kutakaswa ile damu mara saba, halafu atamtangaza mtu huyo kuwa safi. Yule ndege hai atamwacha aende zake mashambani nje ya mji.
8 Huyo mtu atayafua mavazi yake, atanyoa nywele zake, na kuoga; naye atakuwa safi. Baada ya hayo atarudi kambini, lakini atakaa nje ya hema lake kwa muda wa siku saba.
9 Siku ya saba atanyoa nywele zake zote, ndevu na kope za macho yake. Kisha atafua mavazi yake na kuoga, ataoga kwa maji; naye atakuwa safi.
10 “Siku ya nane ataleta wanakondoo madume wawili wasio na dosari, kondoo jike wa mwaka mmoja asiye na dosari, kilo tatu za unga laini uliochanganywa na mafuta kwa ajili ya sadaka ya nafaka pamoja na mafuta theluthi moja ya lita.