11 “Aroni atamtoa fahali wa sadaka ya kuondoa dhambi kwa ajili yake mwenyewe, na kufanya ibada ya upatanisho kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya jamaa yake, kisha atamchinja fahali huyo sadaka ya kuondoa dhambi.
12 Halafu atachukua chetezo na kutwaa makaa madhabahuni mbele ya Mwenyezi-Mungu na ubani konzi mbili uliosagwa vizuri sana.
13 Ili asije akafa, atauleta ubani huo mbele ya Mwenyezi-Mungu na kuutia katika moto ili moshi wa ubani huo ukifunike kifuniko cha sanduku la agano.
14 Atachukua kiasi cha damu ya yule fahali na kunyunyiza kwa kidole chake upande wa mashariki juu ya kiti cha rehema kisha atainyunyizia mbele ya sanduku la agano mara saba kwa kidole chake.
15 “Halafu atamchinja yule beberu wa sadaka ya kuondoa dhambi kwa ajili ya watu wote. Damu ya mbuzi huyo ataileta ndani mahali patakatifu sana na kufanya kama alivyofanya na damu ya yule fahali; atainyunyiza juu ya kiti cha rehema, upande wake wa mbele.
16 Hivyo atafanya ibada ya upatanisho kwa ajili ya mahali patakatifu kwa sababu ya unajisi, makosa na dhambi zote za Waisraeli. Ndivyo atakavyofanya pia kwa ajili ya hema la mkutano lililo miongoni mwa watu hao walio najisi.
17 Wakati Aroni anafanya ibada ya upatanisho kwa ajili yake mwenyewe, jamaa yake na jamii nzima ya Israeli, kamwe asiwepo mtu yeyote ndani ya hema la mkutano hadi atakapokuwa amemaliza na kutoka nje.