3 Kutakuwa na siku sita za kufanya kazi. Lakini siku ya saba ni Sabato; siku hiyo ni ya mapumziko rasmi, hamtafanya kazi na mtakuwa na mkutano mtakatifu. Siku hiyo ya saba hamtafanya kazi; hiyo ni Sabato ambayo ni wakfu kwangu mimi Mwenyezi-Mungu katika makao yenu yote.
4 “Sikukuu zangu nyingine mimi Mwenyezi-Mungu ambazo mtakuwa na mkutano mtakatifu zitafanyika katika nyakati zifuatazo zilizopangwa.
5 “Jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza mtaadhimisha kwa heshima yangu mimi Mwenyezi-Mungu sikukuu ya Pasaka.
6 Siku ya kumi na tano ya mwezi huohuo, sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu itaanza. Kwa muda wa siku saba, mtakula mikate isiyotiwa chachu.
7 Katika siku ya kwanza mtakuwa na mkutano mtakatifu. Siku hiyo msifanye kazi.
8 Kwa muda wa siku hizo zote saba mtanitolea mimi Mwenyezi-Mungu sadaka za kuteketezwa kwa moto. Katika siku ya saba mtafanya mkutano mtakatifu. Msifanye kazi.”
9 Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose,