8 Hakikisha kuwa hutakisahau kamwe kitabu hiki cha sheria; bali kila siku utajifunza kitabu hiki, mchana na usiku, ili upate kutekeleza yote yaliyoandikwa humu, nawe utafanikiwa na kustawi popote uendapo.
9 Kumbuka kuwa mimi nimekuamuru uwe imara na hodari. Usiogope wala usifadhaike kwa kuwa mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, niko pamoja nawe popote uendapo.”
10 Kisha Yoshua akawaamuru viongozi wa watu,
11 “Piteni katika kambi na kuwaamrisha watu watayarishe chakula, kwa kuwa baada ya siku tatu mtavuka mto Yordani, kwenda kuimiliki nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu anawapeni iwe mali yenu.”
12 Yoshua akawaambia watu wa kabila la Reubeni na Gadi na nusu ya kabila la Manase:
13 “Kumbukeni lile jambo ambalo Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, aliwaamuru akisema, ‘Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawapa mahali pa kupumzika, na atawapa nchi hii’.
14 Wake zenu, watoto wenu na wanyama wenu wa kufugwa watabaki katika nchi hiyo ambayo Mose aliwapeni, ngambo ya mto Yordani. Lakini wanaume wote hodari wakiwa na silaha watavuka mto na kuwatangulia ndugu zenu.