7 Lakini Waisraeli wakawajibu hao Wahivi, “Tunawezaje kufanya agano nanyi? Labda nyinyi mnaishi karibu nasi.”
8 Nao wakamwambia Yoshua, “Sisi tu watumishi wako.” Naye Yoshua akawauliza, “Nyinyi ni akina nani, na mnatoka wapi?”
9 Wakamjibu, “Sisi, watumishi wako, tumetoka nchi ya mbali na tumekuja kwa maana tumesikia sifa za jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; tulipata habari za umaarufu wake na yote aliyoyafanya nchini Misri.
10 Tumesikia yote aliyowatenda wafalme wawili wa Waamori waliokuwa ngambo ya mto Yordani, mfalme Sihoni wa Heshboni na mfalme Ogu wa Bashani aliyekaa huko Ashtarothi.
11 Ndipo wazee wetu na wananchi wote wa nchi yetu, wakatuambia, tuchukue posho ya safari, tuje kukutana nanyi na kuwaambia kwamba sisi ni watumishi wenu; tafadhali fanyeni agano nasi.
12 Tazama mikate yetu ambayo ilikuwa bado moto tulipoichukua wakati tulipoondoka kwetu, lakini sasa imekauka na kuota ukungu.
13 Viriba hivi tulivijaza maji vikiwa vipya, lakini sasa vimepasukapasuka. Hata mavazi na viatu vyetu vimechakaa, kwani safari ilikuwa ndefu sana.”