1 Neno la Mwenyezi-Mungu wa majeshi likanijia mimi Zekaria:
2 “Ninawaka upendo mkuu kwa ajili ya Siyoni, na ninawaka ghadhabu nyingi dhidi ya adui zake. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nimesema hayo.
3 Nitaurudia mji wa Siyoni na kufanya makao yangu mjini Yerusalemu. Mji wa Yerusalemu utaitwa ‘Mji Mwaminifu,’ na mlima wangu mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, utaitwa ‘Mlima Mtakatifu.’
4 Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema: Wazee, wanaume kwa wanawake, wataonekana tena wamekaa kwenye barabara za Yerusalemu, kila mmoja na mkongojo wake kwa sababu ya kuishi miaka mingi.
5 Barabara za Yerusalemu zitajaa wavulana na wasichana, wakichezacheza humo.
6 Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema: Kwa watu hawa waliosalia, hali hii inaonekana kuwa kitu kisichowezekana; lakini mnadhani haiwezekani kwangu mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi?