4 Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema: Wazee, wanaume kwa wanawake, wataonekana tena wamekaa kwenye barabara za Yerusalemu, kila mmoja na mkongojo wake kwa sababu ya kuishi miaka mingi.
5 Barabara za Yerusalemu zitajaa wavulana na wasichana, wakichezacheza humo.
6 Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema: Kwa watu hawa waliosalia, hali hii inaonekana kuwa kitu kisichowezekana; lakini mnadhani haiwezekani kwangu mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi?
7 Nitawaokoa watu wangu kutoka nchi ya mashariki na kutoka nchi ya magharibi
8 na kuwafanya wakae katika mji wa Yerusalemu. Wao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao; nitatawala juu yao kwa uaminifu na haki.”
9 Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Jipeni moyo! Sasa mnayasikia maneno ambayo mlitangaziwa na manabii wakati ulipowekwa msingi wa hekalu langu, kulijenga upya.
10 Kabla ya wakati huo, watu hawakupata mshahara kwa kazi zao wala kwa kukodisha mnyama. Hamkuwa na usalama kwa sababu ya adui zenu, maana nilisababisha uhasama kati ya watu wote.