31 Watumwa wake wakamwambia, Angalia sasa, tumesikia ya kuwa wafalme wa nyumba ya Israeli ni wafalme wenye rehema; tafadhali, tuvae magunia viunoni, na kamba vichwani, tumtokee mfalme wa Israeli; labda atakuokoa roho yako.
32 Basi wakajifungia magunia viunoni, na kamba vichwani, wakamjia mfalme wa Israeli, wakasema, Mtumwa wako Ben-hadadi asema Roho yangu, nakusihi, iishi. Akasema, Je! Yu hai bado? Ni ndugu yangu yeye.
33 Wale watu wakaangalia sana, wakafanya haraka kulishika neno hilo kama ni nia yake, wakasema, Ndugu yako, Ben-hadadi. Akasema, Haya! Nendeni mkamlete. Ndipo Ben-hadadi akamtokea, naye akampandisha garini.
34 Na Ben-hadadi akamwambia, Miji ile baba yangu aliyomnyang’anya baba yako nitairudisha; nawe utajifanyia njia huko Dameski, kama baba yangu aliyoifanya huko Samaria. Ahabu akasema, Nami nitakuacha kwa mapatano haya. Akafanya mapatano naye, akamwacha.
35 Basi, mtu mmoja wa wana wa manabii akamwambia mwenzake kwa neno la BWANA, Nipige, nakusihi. Akakataa yule kumpiga.
36 Akamwambia, Kwa sababu hukuisikiliza sauti ya BWANA, angalia, mara ukitoka kwangu simba atakuua. Na mara alipotoka kwake, simba alimwona, akamwua.
37 Ndipo akaona mtu mwingine, akasema, Nipige, nakusihi. Yule mtu akampiga, hata kumpiga na kumtia jeraha.