18 Ee BWANA, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, baba zetu, ulilinde jambo hili milele katika fikira za mawazo ya mioyo ya watu wako, ukaiongoze mioyo yao kwako;
19 naye Sulemani mwanangu, umpe moyo mkamilifu, ili azishike amri zako, na shuhuda zako, na maagizo yako, akayatende hayo yote na kuijenga nyumba hii ya enzi, niliyoiwekea akiba.
20 Ndipo Daudi akawaambia kusanyiko lote, Haya, mhimidini BWANA, Mungu wenu. Basi kusanyiko lote wakamhimidi BWANA, Mungu wa baba zao, wakainama vichwa vyao, wakamsujudia BWANA, na mfalme naye.
21 Wakamtolea BWANA dhabihu, wakamchinjia BWANA sadaka za kuteketezwa, siku ya pili yake, yaani, ng’ombe elfu, na kondoo waume elfu, na wana-kondoo elfu, pamoja na sadaka zao za vinywaji, na dhabihu nyingi kwa ajili ya Israeli wote;
22 wakala na kunywa mbele za BWANA siku ile, kwa furaha kuu. Wakamtawaza Sulemani, mwana wa Daudi, mara ya pili, wakamtia mafuta mbele za BWANA, awe mkuu, na Sadoki awe kuhani.
23 Ndipo Sulemani akaketi katika kiti cha enzi cha BWANA, awe mfalme badala ya Daudi babaye, akafanikiwa; nao Israeli wote wakamtii.
24 Nao wakuu wote, na mashujaa, na wana wote wa mfalme Daudi nao, wakajitia chini ya mfalme Sulemani.